23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Baraza la Madiwani Chemba lataka kuchukuliwa hatua za kinidhamu Afisa Manunuzi

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

BARAZA la Madiwani la Halmashauri Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma limetoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Siwema Hamoud Juma kumchukulia hatua za kinidhamu Afisa Manunuzi wa Wilaya hiyo, Michael Mapera na wasaidizi wake kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya umma katika mambo mbalimbali.

Maelekezo hayo yametolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chemba, Sambala Said wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Madiwani.

Kikao hicho kilipokea uwasilishaji wa Ripoti za kazi za Kamati mbalimbali kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia  Oktoba hadi Desemba 2021.

Mwenyekiti huyo wa Chemba amesema miongoni mwa mambo ambayo yanakwamisha maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Chemba ni kufuatia suala la watu wa manunuzi kuwa na tamaa za kujipatia kipato binafsi bila ya kuzingatia kanuni, sheria na taratibu  walizowekewa.

Amesema kuwa baadhi ya wanunuzi wamekuwa na tabia ya kuwaelekeza wasambazaji kupandisha bei za bidhaa kinyume na bei ya soko kitendo ambacho kinakiuka utaratibu waliojiwekea.

Aidha, amesema katika kikao hicho kuliibuka hoja ya changamoto ya ukusanyaji mapato kwani yameshuka kutoka Sh milioni 153 kwa mwezi Novemba mpaka Sh milioni 106 kwa Desemba kwa mujibu wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango.

Sambala amesema kutokana na changamoto hiyo ya muda mrefu Baraza la Madiwani limemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kulishughulikia suala hilo na  kulikabidhi baraza kwa hatua zaidi za kiutekelezaji.

“Tunataka tufanye kitu ambacho kitafanya watu wafahamu tunataka kuelekea wapi sisi Chemba kama Halmashauri, tunataka kutoka huko tulikotoka ambako hatukuwa tuna taswira nzuri tukusanye mapato ya kutosha ili tutekeleze miradi yetu,’’ amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles