23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Barafu: Kutoka sonara mpaka kuwa nyota wa filamu

suleiman_barafuNa JOHANES RESPICHIUS

KAMA wewe ni mfuatiliaji wa filamu za kibongo, basi jina la Suleiman Abdallah ‘Barafu’ litakuwa si geni masikioni mwako.

Barafu amewahi kuonekana kwenye filamu nyingi, kama vile Shoe Shine, Jamani Mwanangu , Daladala, House Boy, Sindano ya Moto, Pasuko la Moyo, Nesi, Selena, Babylon, Curse of Marriage, One Night,  Last Card,  The Long Story na DNA.

Swaggaz imepata nafasi ya kumuweka kwenye chemba hii ya Gumzo la Town ambapo ameweza kuongelea mambo mengi yanayohusu maisha yake binafsi na ndani ya kazi ya sanaa.

 

HISTORIA YAKE

Anasema alianza kuigiza akiwa bado mdogo, anakumbuka kipindi hicho alikuwa darasa la tatu katika skauti na kila walipokuwa wakienda kambini ‘Camp Fire’ kila mwanafunzi alikuwa anaonyesha kipaji chake na yeye alipenda kuigiza na kuchekesha.

“Baada ya kumaliza darasa la saba sikubahatika kuendelea na sanaa, nilikwenda chuo cha ufundi na hatimaye kufungua kibanda cha sonara.

“Siku moja nilikwenda kwenye uzinduzi wa albamu ya Banza Stone iliyokuwa inaitwa ‘Yuro’ nikakutana na Issa Mussa ‘Cloud 112’, baada ya kukaa naye akaniambia mwonekano wangu unafaa kuigiza na akaniuliza kwanini nisiigize.

“Baada ya hapo alinichukua na kunipa nafasi kwenye filamu yake inayoitwa ‘Security’, nilifanya vizuri kisha nikaanza kwenda kwenye vikundi, safari yangu ikawa imeanzia hapo,” anasema Barafu.

 

CHANGAMOTO

“Changamoto ni nyingi sana kwa sababu kazi ya sanaa ni ngumu, maana mpaka ufikie hatua ya kuitegemea yenyewe kukuingizia kipato lazima jasho likutoke na vikwazo huwa ni vingi sana.

“Sanaa unapoanza sio kama watu wanavyofikiri, maana unapoanza haikulipi, badala yake unakuwa unatumia fedha zako mwenyewe, hivyo inahitaji kujituma na kutokata tamaa,” anasema Barafu.

Pia anasema ugumu wa sanaa unaletwa na mfumo mzima wa maisha uliofanya sanaa isiwe kitu cha kujitolea, bali ni kazi na hauwezi kupata kazi kama hufahamiki.

 

ASITISHA KUTOA FILAMU

Barafu anasema tayari ameachia filamu zake binafsi tatu na sasa amesitisha kufanya hivyo kutokana na kutouelewa mwelekeo wa soko.

“Nilisitisha kucheza filamu baada ya kutoa filamu yangu ya mwisho inayoitwa Daladala. Sababu kubwa ni soko la sinema kuwa kama biashara kichaa, maana unaweza kuwa umefanya kazi ya kukuingizia milioni sita, lakini utahangaika kuipata na unaweza usiipate kwa wakati.

“Hakuna biashara kichaa kama ya sinema, unakuta umetumia fedha nyingi kuitengeneza lakini unakwenda kuikopesha kwa Mhindi na anakaa nayo kwa miezi sita bila kuiuza. Na ukibahatika akaiuza baada ya wiki mbili ndipo anakupa pesa yako tena anakupa nusu.

“Ifikie hatua mtu akitaka kuuza filamu atoe fedha kisha apewe sinema akafanye anavyojua yeye,  mbona ukitaka mkate unatoa hela kwanza halafu unapewa unaondoka zako,” anasema Barafu.

Aliongeza kuwa utafika muda akifanya filamu ataisambaza mwenyewe na ataisambaza kitofauti kwa kusafiri kwenda mikoani kuipeleka filamu yake.

 

KIPI KINAITAFUNA TASNIA HII?

Anasema wapo baadhi ya wasanii ambao wamekuwa wakipeleka maneno na kutoa siri wanazozijadili kwenye vikao vyao. Wasanii hao hupeleka umbea huo kwa wasambazaji, kitu kinachoirudisha nyuma tasnia.

“Inawezekana tukafika hatua ya kulipwa kabla ya msambazaji kwenda kuuza, lakini kinachotukwamisha ni ujinga, umbea na unafiki wa baadhi ya wasanii.

“Wasanii hatuna umoja, tunaweza kufanya kikao chetu na kuazimia mambo fulani, lakini muda mfupi unasikia mtu ameshayapeleka kwa Mhindi na siyo kwamba ni msanii chipukizi anayefanya hivi, ni watu ambao nikiwataja huwezi kuamini.

“Mtu anaona kitendo hicho kina faida kwake, ili aonekane yeye ndiyo wa maana na wenzake wabaya, bila kujua kuwa anajichinja mwenyewe na kufinyanga maendeleo ya sanaa,” anasema Barafu.

 

UPANDE WA SOKA VIPI?

Anasema kabla hajaingia kwenye sanaa watu wengi walimtabiria kuwa atakuja kutoka kupitia soka kutokana na kiwango chake kikubwa cha kucheza mpira.

“Watu wengi huwa hawaamini kama ninacheza filamu kwa sababu walikuwa wanafahamu nina kiwango kizuri kwenye soka, lakini mambo yalibadilika nikaingia kwenye sanaa,” anasema.

“Pia mimi ni shabiki wa Yanga, naipenda timu hii kwa sababu wachezaji wake wanaujua mpira na huwa nawashangaa mashabiki wa Simba wanaposema timu yangu inabebwa wakati wao ndiyo vinara wa fujo. Kama sisi tuna vurugu kipindi wametufunga bao tano tungeng’oa viti vyote,” anasema Barafu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles