24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Barabara ya Tanga-Pangani kikwazo cha maendeleo

barabara

NA OSCAR ASSENGA, PANGANI

MIONGONI mwa mambo ambayo huchangia kwa asilimia kubwa kukwamisha maendeleo kwenye maeneo mengi hapa nchini ni suala la ubovu wa miundombinu iliyopo, kwani ukiangalia ufikaji wake kwa baadhi ya sehemu imekuwa ni changamoto kubwa.

Wilaya ya Pangani ni miongoni mwa wilaya nane zilizopo katika Mkoa wa Tanga ambapo pia unaweza kusema ni kongwe hapa nchini, lakini bado maendeleo yake yamekuwa chini sana na kubwa ambalo tunaweza kueleza linaweza kusababishwa na ubovu wa miundombinu.

Ubovu wa miundombinu ya barabara hiyo unatajwa kuwa ni moja kati ya mambo ambayo yanasababisha kurudisha nyuma maendeleo ya wilaya hiyo
yenye maeneo mengi ya kitalii ambayo yanaweza kutumika kuiingizia Serikali mapato kutokana na makusanyo, hali hiyo imechangia pia wenye magari kutoza nauli kubwa tofauti na ile ya halali iliyopangwa na Sumatra.

Kuna wakati inafikia watu wanaotaka kwenda Wilaya ya Pangani wanalazimika kufika kwa sababu maalumu, ikiwemo sherehe za kifamilia au wakati wanapofiwa na ndugu na jamii kwa wale wanaoishi mbali na Mkoa wa Tanga.

Hivi kwa nini mpaka wananchi wafikie hatua hiyo wakati Serikali ipo na inaweza kutekeleza mpango wa ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani kwa kiwango cha lami na kuweza kuondosha changamoto hiyo kwa wananchi ambao wamekuwa wakiteseka sana, hasa nyakati za mvua?

Najiuliza hali hii kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo mpaka lini? Na nani ambaye anakwamisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wabunge na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo kwa miaka kadhaa bila mafanikio.

Cha kushangaza barabara hiyo ina uwakilishi wa wabunge watatu ambao ndio wananchi wao wamekuwa wakikumbana na changamoto hiyo kubwa, mpaka sasa bado tunaambiwa ni upembuzi yakinifu unafanyika, lakini dalili za kuanza ujenzi wake ni kama vile danganya toto.

Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM), Jumaa Aweso, Mbunge wa Jimbo la Tanga (CUF), Mussa Mbaruku na Mbunge wa Jimbo la Muheza (CCM), Balozi Rajabu Adadi, nawaeleza kwamba wapiga kura wenu wamekuwa wakiteseka na ubovu wa miundombinu ya barabara hiyo.

Ni jukumu lenu kuhakikisha mnapigana kufa na kupona ili kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo, kwani hakuna jingine zaidi ya kuihimiza Serikali kutekeleza kwa vitendo ujenzi wake, kwani kila wakati imekuwa ikielezwa inafanyiwa upembezi yakinifu.

Hali ya ubovu wa barabara hiyo huwezi kuiona kiurahisi katika kipindi cha kiangazi, bali ni pale mvua zinapokuwa zikianza kunyesha, kwani
licha ya kutokupitika, lakini pia imekuwa ikisababisha usumbufu mkubwa kwa abiria.

Pamoja na kuelezea hayo yote, lakini bado nisisitize kuwa umuhimu wa barabara hiyo ni mkubwa kwa kuunganisha Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Pwani, lakini pia itafungua fursa za kiuwekezaji na kiutalii kutokana na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Mto Pangani, ambao hutiririsha maji yake Bahari ya Hindi.

Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli na kauli mbiu yake ya Hapa Kazi tu ione umuhimu wa kusaidia ujenzi

wa barabara hiyo ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wananchi wa wilaya hiyo ambao wamekuwa wakikumbana na adha ya ubovu wa miundombinu.

Tunaomba ikiwezekana Barabara ya Tanga-Pangani ianze kujengwa, kwani itachangia kuongeza pato la Mkoa wa Tanga na nchi kwa ujumla na kuwaondolewa wananchi adha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles