Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
HUKU ikiwa bado haijaanza kutumika, barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (Dart), imeanza kuwekwa viraka, hali ambayo imesababisha msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Mandela na Samnujoma, jijini Dar es Salaam.
Viraka hivyo vimeanza kuwekwa kwenye barabara hiyo eneo la Ubungo ambalo linaunganisha barabara hizo zilizokumbwa na misururu mirefu ya magari jana.
Mradi huo ulitakiwa kukabidhiwa tangu Oktoba mwaka huu ili mabasi hayo yaweze kuanza kazi.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Asteria Mlambo, alisema ukarabati huo umekuja kutokana na dosari zilizojitokeza katika eneo hilo.
“Katika eneo la Ubungo karibu na maungio ya barabara za Morogoro, Mandela na Samnujoma, kuna dosari ndogo ndogo ambazo zinapaswa kufanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kwa mradi huo.
“Kuna baadhi ya maeneo mafundi wanaendelea na ukarabati wa miundombinu iliyoharibika kutokana na dosari ndogondogo zilizojitokeza, hivyo tuwaache wafanye kazi ili waweze kumaliza kwa wakati,”alisema Mlambo.
Aliongeza, awali walishatoa taarifa katika vyombo vya habari juu ya marekebisho hayo na kuwaomba wananchi waache kuuliza maswali ili waweze kuendelea na shughuli zao.
“Tulishatoa maelezo kwenye vyombo vya habari juu ya kinachoendelea kwenye mradi huu, lakini kila siku mnarudi na kuuliza jambo hilo hilo.
“Ninawaomba mtuache tufanye kazi kwa sababu mradi wenyewe haujakabidhiwa, tuna haki ya kuangalia dosari na kuzifanyia marekebisho kabla ya kuukabidhi,” alisema.