27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Barabara ya Kitunda – Msongola kukarabatiwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa jimbo la Ukonga, Jerry Silaa ameahidi kukarabati barabara ya Kitunda mpaka Msongola kupitia Kivule yenye urefu wa kilomita 14.5 ili kuhakikisha inapitika wakati serikali ikijipanga kuijenga kwa kiwango cha lami.

Akizungumza katika mahafali ya tatu ya wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Serengeti, Silaa amesema barabara hiyo ilishaanza kuwekwa lami eneo la Kitunda ambayo ni kilomita 3.2.

Amesema wakati wanajipanga kuweka kipande kilichobaki kilomita 11.3 atahakikisha inapitika ili kuwasaidia wananchi kufika katika shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi.

“Niliona ujumbe kwenye kundi la WhatsApp mtu mmoja anasema mwambieni mbunge atutengezee barabara fedha za kula tutatafuta wenyewe, ule ujumbe ulinigusa nikakumbuka tunavyodai hivi vitu bungeni, unajua sisi wabunge wa mjini huwa tunawaambia bungeni wananchi wetu hawahitaji pembejeo, hakuna mtu anahitaji mbolea wala bei ya mazao.

“Huwa tunawaambia watu wa mjini wanahitaji barabara kwa sababu maisha yao ni kusafiri kwenda kutafuta fedha, wakulima wakituletea mazao tunanunua kwa bei zao kwa hiyo sisi wa mjini tunahitaji barabara tu,”amesema Silaa.

Amesema pamoja na ukarabati atakaofanya lakini serikali imejipanga kutatua kero hiyo kwa kujenga kwa kiwango cha lami na kwamba utekelezaji wake tayari umeshaagizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2020 -2025.

“Viongozi wenzangu wakati tunasubiri utekelezaji tuhakikishe barabara zinapitika, tufanye marekebisho ambayo yatawafanya wananchi wetu waweze kufanya safari zao za kila siku,” amesema.

Kuhusu msaada wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo unaofanya na Mamlaka ya Elimu (TEA) amesema amekuwa akiguswa na changamoto zilizopo katika shule zote za jimbo hilo ambapo katika Kata ya Kivule Shule za Msingi Serengeti na Kivule zitapata majengo hayo.

“Tumepata ufadhili kutoa TEA ambapo watajenga madarasa matatu katika Shule ya Msingi Serengeti na mengine matatu na matundu 24 ya vyoo katika Shule ya Msingi Kivule,” amesema Silaa.

Amesema pia ofisi ya mbunge katika bajeti yake ya mwaka huu itajenga choo kimoja cha walimu katika Shule ya Msingi Serengeti ambayo kwa sasa wanatumia vyoo vya wanafunzi, darasa moja la watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na kununua meza za walimu lengo likiwa ni kusaidia kuinua elimu.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Serengeti, Bihimba Mpaya, amesema shule hiyo yenye wanafunzi 2,600 imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo madarasa na matundu ya vyoo hasa vya walimu.

Amemshukuru mbunge huyo kwa kusikia kilio hicho na kuahidi kusaidia harakati za kuinua elimu ikiwemo kuahidi kujenga miundombinu ya shule.

Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 252 wamehitimu na kati yao wavulana ni 128 na wasichana ni 124.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles