31.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 18, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Bandari ya Dar yapunguza muda wa ushushaji wa mizigo, yazidi kuimarisha ufanisi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Galusi, amesema maboresho yaliyofanyika bandarini yamesababisha kupungua kwa muda wa kushusha na kupakua mizigo kutoka siku 10 hadi siku tatu, huku akihimiza wafanyabiashara kufuata mizigo yao kwa wakati ili kuondoa mlundikano.

Galusi alitoa kauli hiyo Januari 15, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) waliotembelea bandari hiyo kujionea shughuli za upakiaji na ushushaji wa mizigo.

“Ujio wa kampuni za DP World na Adani Ports umeleta mabadiliko makubwa, muda wa kusubiri mizigo bandarini umepungua kwa kiasi kikubwa. Tunawaomba wateja wetu waje kuchukua mizigo kwa wakati kwani sasa kuna mlundikano mkubwa wa mizigo,” alisema Galusi.

Aliongeza kuwa uingizaji wa mizigo umeongezeka kwa asilimia 60 kwa nchi jirani kama Congo, Zambia, na Rwanda, na kwa asilimia 40 kwa mizigo ya ndani, hatua inayoongeza ushindani wa bandari hiyo kimataifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JWT, Hamis Livembe, alisema ufanisi wa bandari unaimarisha biashara na kuvutia wateja kutoka nchi jirani. “Bandari sasa imeboresha huduma kwa kiwango kikubwa. Kushusha mzigo sasa kunachukua siku tatu tu, tofauti na hapo awali ambapo ucheleweshaji ulikuwa unachukua hadi siku 40. Hii imeongeza fursa kwa wafanyabiashara kuleta mizigo zaidi kwa haraka,” alisema Livembe.

Meneja wa Uhusiano wa DP World, Elitunu Mallamia, alisema kampuni hiyo imeongeza ufanisi kwa kushughulikia meli 27 na makontena zaidi ya 220,000 katika mwezi wa Desemba 2024 pekee.

“Tunaendelea kuvunja rekodi kwa kuhudumia mizigo kwa wakati, lakini changamoto ni wateja kuchelewesha kuchukua mizigo yao. Tunatoa wito kwa wateja kuondosha mizigo mapema ili tuweze kushughulikia mizigo mingine zaidi,” alisema Mallamia.

Maboresho haya yanayofanywa bandarini yanalenga kuongeza kasi ya ushushaji mizigo na kuboresha huduma, hatua ambayo inaongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika kanda ya Afrika Mashariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles