Na Florence Sanawa, Mtwara
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), mkoani Mtwara imetoa msaada wa shuka 100 zenye thamani ya zaidi ya Sh 1.3 kwa Hospitali Rufaa Ligula.
Akipokea shuka hizo Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo. Dickson Sahini amesema hospitali hiyo ina vitanda 248 ambapo vinatakiwa kuwa na shuka nane kwa kila kitanda hali ambayo inakuwa ngumu kutokana na uhaba uliopo hospitlaini hapo.
Amesema awali hospitali hiyo ilikuwa na upungufu wa shuka 900 ambapo baada ya kupata hizo wamebaki na upungufu wa shuka 800 ili kupata shuka nane kwa kila kitanda kama taratibu zinavyotakiwa kuwa.
“Mashuka ni sehemu ya mahitaji katika hospitali yetu tunatambua zipo taasisi mbalimbali zinaweza kutusaidia kutatua changamoto zinazotukabili mbali na mashuka ikiwamo uboreshaji wa majengo ambayo hivi sasa ni chakavu, tuna tatizo kubwa la uhaba wa vifaa tiba, vifaa vishirikishi ikiwamo mashine ya kufulia,” amesema Sahini.
Kwa upande wake Mkuu wa Bandari Mkoa wa Mtwara, Nelson Mlali amesema mamlaka hiyo imeamua kutoa shuka hizo kuisaidia jamii inayoizunguka na kuikumbusha kuitembelea bandari hiyo ili kufahamu shughuli zinazofanyika katika eneo hilo.