Na MWANDISHI WETU- DAR ES SALAAM
RAIS wa wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nchini Tanzania, Sumaili Edward, ametangaza kuwa wafanyabiashara wa nchi hiyo wataanza tena kupitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam Oktoba 30, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Edward alisema awali bandari hiyo ilikuwa na changamoto nyingi zilizosababisha washindwe kuitumia.
Alisema wanapojipanga kuanza kutumia bandari ya Dar es Salaam, wanaishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaondolea vikwazo walivyokuwa wakikabiliana navyo.
“Tumekaa zaidi ya miaka miwili bila kutumia bandari hii kutokana na vikwazo vilivyokuwa nje ya uwezo wetu, moja tatizo la mizani, stoo ya kuhifadhia bidhaa pia tulikuwa hatupati faida kwani kazi ya siku moja ilikuwa inachukua wiki nzima.
“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kusikia kilio chetu. Awali katika bandari hii tulikuwa tunapewa siku 14 za kuhifadhi mizigo lakini hivi sasa siku 30 kwani kuanzia Novemba mwaka huu bandari itasheheni mizigo mingi sana,” alisema Edward.