BALOZI WA URUSI UN AFARIKI DUNIA

NEW YORK, MAREKANI


BALOZI wa Urusi katika Umoja wa Mataifa (UN), Vitaly Churkin, amefariki dunia ghafla akiwa kazini mjini hapa juzi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imethibitisha kifo cha Churkin, ambaye angetimiza miaka 65 jana, ingawa chanzo chake bado hakijabainika.

Churkin amehudumu kama balozi wa Urusi katika UN tangu 2006 ambako alijizolea sifa kama mtetezi wa dhati wa sera za nchi yake.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameeleza kusikitishwa na kifo cha balozi huyo aliyemtaja kuwa na kipaji kikubwa kidiplomasia.

Runinga ya taifa ya Urusi, Rossiya24, ilimsifu kwa kuwazidi nguvu wapinzani wake na mara nyingi kuwaacha wakiwa ‘hawana la kusema’.

Wengi wa wapinzani hao wamekuwa pia wakituma salamu za rambirambi wakimweleza balozi huyo kama mtu waliyemheshimu licha ya kutokubaliana naye kimisimamo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here