Na Mwandishi wetu, Shinyanga
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, amewaonya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za kujiepusha na matumizi ya fedha katika kutafuta nafasi za uongozi kwani kufanya hivyo ni kukiuka katiba ya chama.
Alisema kuna baadhi ya watu wenye nia ya kugombea uongozi lakini badala ya kwenda wenyewe wanatuma watu wengine kutoa rushwa na kusema wana taarifa zao na watawashughulikia ipasavyo.
Alisema wakati wa ziara yake ya kichama mkoani Shinyanga alipokutana na viongozi wa CCM Mkoa na Wilaya ya Kahama, yeye akiwa ni mlezi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
‘’Kiongozi yoyote anayetafuta uongozi kwa kununua huyo sio kiongozi mzuri, uongozi hautafutwi kwa kununua, utafutwa kwa kujenga hoja,’’alisema.
Alisema Serikali iko macho kuwabaini wote wanaotaka kutumia ushawishi wa fedha kujipatia uongozi kwani macho yake yanaangaza kila mahali na wana uhakika wataonekana pasiposhaka.
Aliwataka wapiga kura wa chama hicho kupokea fedha watakazopewa na wataka uongozi lakini wasije wakawapa kura zao.
Aliwataka wabunge wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea na kazi ya kukamilisha ahadi zao kwa wananchi kwani bado ni viongozi hadi zoezi la kuchukua fomu litakapoanza ingawa inawezakena baadhi yao wanaweza kuwa wanamaliza muda wao na wengine kupoteza nafasi za uongozi kwa kushindwa katika kura za maoni.