30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI SEIF AKOSHWA NA MRADI WA TASAF

Na Estom Sanga- Zanzibar


MAKAMU wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema mchango unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf katika kuhamasisha wananchi kupambana na umasikini, unapaswa kuungwa mkono kwani unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali zote mbili za kuwaondolea wananchi kero ya umasikini.

Balozi Iddi ametoa kauli hiyo alipokutana na baadhi ya wadau wa Maendeleo na Maofisa wa Tasaf mjini Unguja, baada ya viongozi na wadau hao wa maendeleo kuhitimisha ziara ya kuwatembelea Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini kisiwani humo.

Alisema mafanikio makubwa yanayojitokeza katika nyanja za elimu, afya na ongezeko la shughuli za kiuchumi miongoni mwa walengwa wa mpango huo, ni ushahidi tosha kuwa wananchi hususani wale ambao wamekuwa wakikabiliwa na umasikini, wanahitaji kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa shughuli za mpango huo ambao umekuja kwa wakati hasa kutokana na ukubwa wa tatizo la umasikini nchini.

“Kwa kutambua hili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono utekelezaji wa shughuli za Tasaf kisiwani humo na kuwataka wananchi hususani wale walioko kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kutumia fursa hiyo vizuri ili hatimaye waweze kuboresha maisha yao,” alisema Balozi Seif.

Akizungumza katika kikao hicho,  Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, alisema hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuweka msukumo wa kutosha katika utekelezaji wa mpango huo zimeendelea kuzaa matunda, ambapo katika maeneo mengi nchini walengwa wameonyesha kuanza kubadilika kwa kuboresha maisha  yao.

Kwa upande wake, Msimamizi wa shughuli za Tasaf katika Benki ya Dunia, Muderis Mohamed, alisema wadau wa maendeleo wameonyesha kuridhishwa na matokeo mazuri yaliyoanza kuonekana kwa kaya za walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini, jambo linaloendelea kuwavutia wadau wengi kujitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya mpango huo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles