28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Balozi Mahiga amtetea Mkewe

Dk. Augustine MahigaNa Bakari Kimwanga, Dodoma

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, amezungumzia sakata la mke wake kudaiwa kumtukana askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Akizungumza na MTANZANIA jana mjini hapa, Dk. Mahiga alisema kwamba mke wake alipishana kauli na askari huyo aliyefahamika kwa jina la Deogratius Mbango, na hakutoa lugha ya matusi kama inavyodaiwa.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, alifuatilia ili kujua ukweli, ikiwamo kusikiliza sauti ya majibizano baina ya askari huyo na mkewe, ambapo alibaini kuwa walipishana kauli.

Hata hivyo Balozi Mahiga alisema suala hilo kwa sasa limemalizika na asingependa kuingia kwenye malumbano zaidi kwa jambo lililopita.

“Ni kweli mama (mke wake) alikuwa katika barabara ya Namanga, ambako alipishana kauli na askari wa usalama, nami nilifuatilia suala hili kwa undani sana. Ninachoweza kusema sitaki kuingia kwenye malumbano juu ya suala hili kwa kuwa limemalizika.

“Wewe umesikiliza hiyo ‘clip’ (sauti ya mazungumzo) je, umesikia neno tusi? Hilo ndilo ninalojua kwa sasa, mengine sijui yanayoendelea,” alijibu kwa kifupi Balozi Mahiga.

Alipoulizwa kuhusu kusambaa kwa picha inayomdhalilisha, Dk. Mahiga alisema kwamba alishangazwa na picha hiyo huku akishindwa kuelewa lengo la watu walioitengeneza na kuisambaza.

“Hata mimi sijui lengo lao nini kuisambaza ile picha, maana mimi niliiona kama ulivyoiona wewe,” alisema.

Picha ya Balozi Mahiga inayoonyesha suruali yake imelowa sehemu ya mbele, imekuwa ikizunguka katika mitandao ya kijamii kwa takriban wiki moja sasa.

 

RAIS MAGUFULI

Rais Dk. John Magufuli alimuagiza Kamishina wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu kumpandisha cheo trafiki huyo ikiwa ni tuzo ya kutukanwa akiwa kazini.

Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akifungua kikao cha makamanda wa polisi wa mikoa kilichofanyika mjini Dodoma.

Rais Magufuli alisema tayari ameshamwonya waziri ambaye mke wake alimtukana askari huyo.

“Hakuna kiongozi au familia ya kiongozi iliyoko juu ya sheria,” alisema Rais Magufuli.

Katika sakata hilo, mke wa Balozi Mahiga anadaiwa kumtukana askari huyo ambaye alikuwa katika kituo chake cha kazi akitekeleza majukumu yake.

Mapema juzi asubuhi, kwenye mitandao ya kijamii ilisambazwa sauti ya mahojiano baina ya askari huyo, mkuu wake wa kazi pamoja na mke wa Mahiga.

Katika sauti hiyo, alisikika askari huyo akilalamikia kitendo cha mke wa Mahiga kumtusi pale alipotaka kumwandikia faini dereva wake kwa kosa la kusimamisha gari katika alama ya pundamilia inayotumika kuvukia watembea kwa miguu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles