BALOZI ‘CISCO’ MTIRO KUZIKWA KESHO DAR

0
551

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


ALIYEKUWA Mkuu wa Itifaki Ikulu, Balozi Abdul ‘Cisco’ Mtiro, amefariki dunia jana katika Hospitali ya Aghakhan alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Adam Mtiro, aliliambia MTANZANIA jana kuwa mazishi ya kaka yake yatafanyika kesho saa saba mchana katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Alisema mwili wa marehemu utawasili nyumbani kwake Mikocheni majira ya saa tano asubuhi na kisha kufanyiwa kisomo, kuswaliwa na baadae kuelekea makaburi  ya Kisutu kwa mazishi.

“Mwili wa marehemu utawasili hapa nyumbani saa 5 asubuhi na kufanyika kisomo,  saa 6:30 mchana tutaelekea makaburi ya Kisutu kwa mazishi,” alisema Adam.

JPM amlilia

Kutokana na msiba huo, Rais Dk. John Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Aziz Mlima, ilieleza kuwa Rais Dk. Magufuli, ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na mabalozi kwa kuondokewa sio tu na ndugu wa karibu  bali na mwanadiplomasia mahiri nchini.

Alisema mchango wa Balozi Mtiro ulikuwa bado unahitajika  katika nyanja za kidipolomasia nchini na duniani.

Mrema amzungumzia Sisco

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Temeke,  Augustine Lyatonga Mrema, alisema ameupokea msiba wa Mtiro kwa masikitiko kwani wakati wa uhai wake alikuwa kijana mzuri na mwenye kuipenda nchi yake.

Mrema alikumbuka kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Temeke mwaka 1996, akiwa NCCR-Mageuzi alipambana na Mtiro wa CCM, huku akisema alikuwa kijana  mzuri ambaye alitoa changamoto kwenye uchaguzi huo.

“Alinipa changamoto kwenye mikutano lakini alikua ni kijana asiyekuwa na makuu kwani alikuwa hatukani na siasa zake zilikuwa za kistaarabu.

“Nawapa pole wanachama wa CCM hasa wa Temeke na wanamichezo kwa kuwa wamempoteza mtu aliyekuwa shupavu ,” alisema Mrema.

Balozi ‘Cisco’ aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Malaysia, Phillipines, Cambodia na Singapore.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here