ASHA BANI na LEORNAD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
MARAIS Wastaafu, Alhaji Ali Hassan Mwinyi wa awamu ya pili na Jakaya Kikwete wa awamu ya nne, jana waliongoza mazishi ya aliyekuwa mkuu wa Itifaki, Balozi Abdulkarim Mtiro ‘Cisco’.
Alizikwa jana katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, ambako mamia ya wanasiasa na watu maarufu walihudhuria.
Balozi Mtiro alifariki Juni 5 , mwaka huu katika Hospitali ya Aghakhan.
Akisoma wasifu wa marehemu, ndugu wa Balozi huyo, Said Ibrahimu alisema ‘Cisco’ alikuwa mtu wa watu aliyependwa na kila mtu.
Alisema alizaliwa Novemba 25, mwaka 1950 Gerezani Kariakoo na baadaye kuhamia Temeke alikoanza shule ya msingi.
Ibrahimu alisema ‘Cisco’ alifaulu masomo yake ya darasa la saba na kujiunga na sekondari ya Agakhan Boys kabla ya kujiunga na Chuo cha Biashara (CBE) na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baadaye aliajiriwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ambako alifanya kazi katika idara mbalimbali.
“Baadaye alikuwa Mkuu wa Itifaki ambako aliweza kuhudhuria na kuongoza mikutano mbalimbali ikiwa ni pamoja na mapokezi ya Rais wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela ‘Madiba’ na kuandaa mkutano mkubwa wa kwanza wa Jumuia ya Madola.
“Baadaye alichaguliwa kuwa balozi katika nchi mbalimbali kabla ya kurejea nchini,’’ alisema Ibrahimu.
Marehemu ameacha mke na watoto wane, wa kike watatu na mmoja wa kiume.
Balozi Cisco pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Malaysia, Phillipines, Cambodia na Singapore
Akitoa salamu za rambirambi katika msiba huo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir, alisema ni msiba mkubwa kwa watu wote na kwamba ni mambo ya Mungu ambaye ameamua kumwita ‘Cisco’.
Alisema kufa ni lazima kwa kila mtu kwa kuwa ni utaratibu na kila mmoja atarudi katika njia hiyo hiyo..
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Musa Salum alisema mauti siyo mwisho wa maisha.
Alisema anaamini kuna maisha baada ya kufa na kwamba adhabu ya kaburi ipo na neema pia ipo.
Mbali na marais wastaafu, viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernad Membe na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Alhaji Adam Kimbisa.
Wengine ni Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete, Balozi Juma Mwapachu na viongozi wengine.