MADRID, HISPANIA
MSHAMBULIAJI, Bale akubali yaishe Madrid ameamua kuondoka Real Madrid kwenda kujiunga na Klabu ya China Jiangsu Suning kwa mkataba wa miaka mitatu.
Vyanzo vilivyo karibu na mshambuliaji huyo raia wa Wales vilithibitisha ripoti kwamba Bale amekubali kuondoka Santiago Bernabeu, ingawa uhamisho huo bado haujakamilika.
Bale amejikuta matatani na kocha wake, Zinedine Zidane ambaye ameonyesha wazi wazi kutomuhitaji katika kikosi chake.
Zidane amekuwa akitamka wazi kuwa Bale kuondoka itakuwa bora kwake, kwani hayupo katika mipango yake ya siku zijazo.
Bale ameahidiwa kuwa mchezaji atakayelipwa zaidi duniani akitua China, kwani atakuwa akilipwa mshahara wa pauni milioni moja kwa wiki(ambazo ni sawa na zaidi ya bilioni 2 za Tanzania).
Licha ya mshambuliaji huyo kutokea benchi kwenye mchezo na kuisadia Real Madrid kushinda kwa penalti 3-2, baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Arsenal kwenye mchezo kujipima nguvu, Zidane alisisitiza hakuna kilichobadilika kwa mchezaji huyo.
Bale alijiunga na Madrid kwa ada ya uhamisho iliyovunja rekodi wakati huo ya pauni milioni 85 kutoka Tottenham Spurs miaka sita iliyopita, akiipuku rekodi ya Cristiano Ronaldo aliyejiunga na timu hiyo kwa pauni milioni 80, akitokea Manchester United mwaka 2009.
Mshambuliaji huyo amebakiza mkataba wa miaka mitatu na mabingwa wao wa kiistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ameshinda mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya , taji moja la La Liga, Copa del Rey, mataji matatu ya Uefa Super na matatu ya Klabu Bingwa ya Dunia.
Bale amefunga mabao matatu katika michezo minne ya fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo Real ilishinda taji hilo mwaka 2014, 2016, 2017 na 2018.
Moja ya sababu kubwa inayomfanya Bale kushindwa kutema cheche Madrid ni majeraha ya mara kwa mara ambayo yamemsababishia kupata fursa ya kuanza katika michezo 78 tu ya Ligi Kuu kwa misimu yote minne.
Msimu uliopita, Bale alifanikiwa kucheza mechi 42 za Real Madrid, huku muda mwingi akiwa nje ya uwanja akiuguza majeraha .
Kurudi kwa Zidane katika kikosi cha Real kulitafsiriwa kama habari mbaya na wakala wa mchezaji huyo, Jonathan Barnett kwa sababu Mfaransa huyo hakutaka kufanya kazi na Bale kwani wanaume hao wawili hawapikiki chungu kimoja.
Bale alianza maisha yake ya soka katika klabu ya Southampton, akiwa na umri wa miaka 16 kabla ya kuondoka katika klabu hiyo mwaka 2007 na kujiunga na Tottenham
Alitumia misimu sita kwenye klabu hiyo ya kaskazini mwa London kabla ya kujiunga na Madrid.
Hata hivyo, Bale amekuwa akihusishwa kurudi katika klabu ya zamani ya Tottenham Spurs, huku pia Manchester United na Bayern Munich zikiwa miongoni mwa timu zilizotamani kumnasa.