Na WAANDISHI WETU
MAPENDEKEZO ya Serikali ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mwaka wa Fedha wa 2017/18 yaliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, yametoa taswira ambayo inaonyesha serikali imetumia hesabu kali kuhakikisha inatanua wigo wa ukusanyaji wa kodi.
Katika hesabu hizo, inaelezwa imeonekana kuleta nafuu kwa upande fulani wa watu wachache na kupeleka maumivu kwa upande mwingine ambao unabeba idadi kubwa ya watu.
Eneo kubwa ambalo si tu linatajwa, huenda si tu likaiongezea mapato makubwa serikali, bali pia kuwapa baadhi nafuu na wakati huo huo kumsababishia maumivu makali mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi, ukiacha lile la ukusanyaji wa kodi ya nyumba zote, ni uamuzi wake wa kuhamishia ada ya mwaka ya leseni ya magari (Road License) kwenye nishati ya mafuta.
Ada hiyo kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, sasa imewekewa mbadala wake wa kulipwa kupitia ushuru wa Sh 40 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, tofauti na sasa ambapo inalipwa kwa mkupuo, tena kulingana na ukubwa wa gari.
AHUENI/UGUMU WAKE
Akisoma mapendekezo ya Serikali, Dk. Mpango alisema Serikali inadhamiria kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari iliyokuwa inalipwa hata kwa magari ambayo hayatumiki.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa na sura mbili hasi na chanya, ya kwanza ni serikali kuongeza mapato kwa maana kwamba inaweza kuhamasisha watu wengi kutumia magari waliyokuwa wameyaacha majumbani mwao kwa muda mrefu kwa sababu ya kukosa fedha za mkupuo kuyalipia ada.
Si hilo tu, vilevile njia hiyo ya kulipia ada hiyo kidogo kidogo inatajwa kumpa urahisi mmiliki wa gari, tofauti na ile ya mkupuo iliyokuwa ikitozwa kwa ulazima.
Baadhi wanaufananisha mfumo huo mpya wa ulipaji wa kodi ya leseni za magari na ule wa malipo ya umeme kupitia mita za Luku, ambako mlaji anakatwa kodi mbalimbali.
Kwamba ili kupata umeme, lazima ununue umeme, hivyo hivyo ili gari liweze kutembea lazima mafuta yanunuliwe na hapo ndipo kodi itakuwa inalipwa moja kwa moja.
Urahisi mwingine ambao unaangukia kwa wamiliki wa magari ambao ni wachache ukilinganisha wale ambao hawana ni kwamba, ada hiyo sasa watalipa kulingana na matumizi yao ya mafuta (ukitumia zaidi utalipa zaidi, ukitumia kidogo utalipa kidogo).
Uchambuzi wa kimahesabu uliofanywa na gazeti hili, kupitia taarifa za wamiliki mbalimbali wa magari madogo hadi makubwa, unaonyesha kuwa kwa matumizi ya chini kwa magari yenye injini ya kuanzia CC 1501 hadi 2500 wanaweza kujikuta ama wanalipa kodi hiyo zaidi au kidogo, ukilinganisha na ile ya mkupuo inayolipwa sasa.
Gloria Kambimtoni anasema yeye anamiliki gari lenye CC 1720 na kwamba analazimika kulipa ada hiyo kila mwaka Sh 180,000.
“Nimepiga hesabu kwa mwezi natumia gharama ya petroli kati ya Sh 200,000 – 250,000, sasa nikiongeza hiyo Sh 40 makato ya mwaka mzima ya ada hiyo itakuwa wastani wa Sh 60,000 tu badala ya 180,000 ninayolipa,” alisema.
UGUMU WAKE
Katika uchambuzi wake, gazeti hili limebaini kuwa, staili mpya ya ulipaji wa ada hiyo inaweza kuwabana zaidi wale wenye matumizi makubwa ya mafuta, ambao sehemu kubwa ni magari ya kibiashara kama daladala na malori ya mizigo na hivyo kumsababishia ugumu mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi.
Dereva wa gari aina ya Fuso aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Juma, ambaye hufuata mazao ya kilimo mkoani Kilimanjaro, alisema kama kodi ya mafuta itaongezwa, ni wazi na yeye atamwongezea gharama za ubebaji mkulima.
“Ni rahisi tu, kama mafuta yatapanda na mimi nitapandisha gharama za ubebaji, kwa maana hiyo mkulima naye atalazimika kufidia pengo kwenye mazao yake,” alisema.
Mmiliki wa gari aliyejitambulisha kwa jina la Bagheshi, ambaye anafanya biashara ya kubeba mizigo kati ya Bariadi-Mwanza au Mara, aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa, ikitokea gari lake ikawa na matumizi madogo, basi atajikuta anainyonya serikali, jambo ambalo alilisifu.
“Kwa kweli nimefurahia kuitoa kodi hii na kuipeleka kwenye mafuta, najua ninakatwa huko, lakini siumii sana kwa sababu siilipi kwa mkupuo. Najua nitakamuliwa sana kama nitakuwa na matumizi makubwa ya gari langu,” alisema Bagheshi.
Kulwa Hassan, ambaye ni dereva wa gari aina ya Toyota Coaster (daladala) ambayo hufanya biashara ya kubeba abiria kutoka Makumbusho hadi Posta, jijini Dar es Salaam, alisema kuanzishwa kwa kodi hiyo kwenye mafuta kunamtolea mzigo mmiliki wa gari na kumshushia dereva na kondakta wake.
“Kawaida mmiliki anapokukabidhi gari yake anakujazia tanki ya mafuta ufanye biashara, lakini inapofika jioni lazima uhakikishe unairejesha gari kwa mmiliki ikiwa imejazwa mafuta kama ulivyoikuta asubuhi, sasa kinachonitia hofu kama nauli zisipoongezwa basi sisi madereva itatushinda, kwa sababu mmiliki hawezi kunielewa kumpa makusanyo yaliyopungufu kufidia pengo la mafuta,” alisema Hassan.
Msomi wa uchumi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam, Dk. Prosper Ngowi, katika uchambuzi wake anasema bajeti hiyo imeleta ahueni kwa wakulima, baada ya kufuta kodi katika mazao kilimo, japokuwa kodi hiyo ni wazi kuwa italipwa na mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hiyo.
“Hii kodi ya mazao itarudi kwa mlaji kwa nini? Mkulima anaweza asikatwe kodi, lakini wakati wa kusafirisha akakumbana na kodi ya magari inayopitia kwenye mafuta, hivyo katika hesabu zake ili apate faida lazima aongeze bei ya mazao, hapa atakayeumia ni mlaji na si mwingine,” alisema Profesa Ngowi.
Alisema mbali na hilo, bajeti hiyo pia imepunguza vyanzo vya mapato vya halmashauri, hivyo kuna haja ya wahusika kutafuta vyanzo vipya vitakavyowaingizia fedha.
KODI YA PIKIPIKI, BAJAJI ZAREJEA KIAINA
Katika kudhihirisha kuwa Serikali imetumia hesabu kali katika kupanua wigo wake wa ukusanyaji kodi katika ya mwaka wa fedha 2017/18, ni hatua yake ya kurejesha kiaina kodi za pikipiki za magurudumu mawili na matatu (bajaji) ambazo awali ilitangaza kuzifuta.
Ikumbukwe katika bajeti inayomaliza muda wake, serikali ilifuta ada ya mwaka ya leseni za vyombo vya moto kama matrekta, pikipiki na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) japokuwa zilipaswa kulipa ada ya ukaguzi wa vifaa vya zimamoto ambayo ni shilingi 10,000 tu katika bajeti .
Katika mapendekezo ya bajeti ya 2017/18, vyombo hivyo vya moto sasa vitalazimika kulipa ada ya leseni ya mwaka kupitia tozo ya Sh 40 kwenye kila lita ya mafuta ya ama petroli au dizeli.
Mbali na vyombo hivyo, pia mitambo mbalimbali inayoendeshwa kwa nishati ya mafuta, mfano majenereta nayo yatalazimika kulipia ada hiyo ya Sh 40.
BAJETI KUUMIZA SERIKALI ZA MITAA
Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniphace Jacob, amesema bajeti kuu ya Serikali ya mwaka mpya wa fedha 2017/18 itaumiza zaidi Serikali za mitaa kwa kuzinyang’anya vyanzo vyake vya mapato, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kodi ya mabango na nyumba za kulala wageni.
“Baada ya bajeti iliyopita kuondoa kodi ya majengo na kuipeleka TRA, wameondoa tena hizi walizoeleza jana ambavyo vilikuwa vinasaidia halmashauri kupata fedha. Wajaribu kufikiria hilo kabla ya kulitekeleza,” alisema Jacob.
WAKULIMA WASIFU/WAHOFU
MTANZANI Jumamosi lilizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya PAAES, ambayo inashughulikia utunzaji wa mazingira, kilimo na ufugaji, Wiliam Ntawundi, ambaye alisema kuwa bajeti hiyo itakuwa mkombozi kwa wakulima na wafugaji endapo itatekelezwa.
Alisema kusamehe kodi ya ongezeko la thamani ‘VAT’ katika vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini na mashine ya mayai ya kutotoleshea vifaranga itakuwa ni hatua kubwa kwa wafugaji na wale waliokuwa na maono na nia ya kufuga.
“Changamoto mojawapo iliyokuwa ikiwasumbua wafugaji, hasa wa kuku ni ulishaji, bei ilikuwa ikipanda mara kwa mara, lakini kwa kuondolewa kodi ya ongezeko la thamani tunaamini bei inaweza ikawa nafuu.”
Kuhusu kuwatambua wafanyabiashara ndogondogo, wakiwamo wauza mboga, Ntawundi alisema hiyo itawasaidia si tu wakulima, bali hata wauzaji wenyewe na serikali.
“Kwa kuwatambua wauza mboga kutawafanya kuaminiwa na taasisi za kifedha, hata watakapotaka kupata mikopo itakuwa ni rahisi kwao, hivyo itawarahisishia kuchukua biashara zao ndogondogo kama mboga na hata kuanzisha mashamba yao wenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Anna Joseph alisema mashine za kutotoleshea ni muhimu kwa mfugaji yeyote anayefanya ufugaji biashara, hivyo kuondoa VAT katika mashine hizo kutawasaidia wafugaji wadogo wadogo.
“Kila mfugaji ana dhamira ya kuwa juu kiuchumi na mashine ya kutotoleshea kwa sisi wafugaji wa kuku ni muhimu, hivyo tumeipokea bajeti kwa furaha, tunaomba tu mambo yasije yakageuka, maana sisi Watanzania tunajua kuongea, lakini kutekeleza ni shida,” alisema.
WAPINZANI WAKESHA
Kwa upande wake, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imeahidi kutoa msimamo kesho kuhusu Bajeti ya Serikali iliyosomwa juzi na kusisitiza kuwa bado hawajaikubali katika baadhi ya mambo.
Akizungumza na gazeti hili, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde, alisema kwa sasa bado wanaisoma na kuitafakari bajeti hiyo, ambapo wamejipanga kutoa maoni ya pamoja siku ya Jumapili mjini Dodoma.
“Jana (juzi) tumejifungia hatujalala, tunachambua hotuba ya bajeti na kuandaa press statement (taarifa kwa vyombo vya habari) kuelezea uchambuzi na msimamo wetu kama kambi ya upinzani, kwa sasa siwezi kuongea zaidi, lakini tutatoa taarifa kamili Jumapili (kesho),” alisema Silinde.
Alisema kambi rasmi ya upinzani haijakubaliana na mambo mengi yaliyopo kwenye bajeti, ikiwamo kupunguza tozo za mazao na kuongeza kodi kwenye mafuta.
Habari hii imeandaliwa na Evans Magege, Aziza Masoud na Grace Shitundu.