24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bajeti ya ulinzi yaongezeka kwa Sh bilioni 286

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeidhinishiwa bajeti ya Sh trilioni 2.14 ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 286, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha unaoisha ambayo ilikuwa Sh trilioni 1.854 . 

Kati ya fedha hizo zilizoidhinishwa na Bunge jana, Sh trilioni 1.726 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida, na Sh bilioni 128 kwa matumizi ya maendeleo. 

Wizara hiyo iliomba kuidhinishiwa zaidi ya  Sh trilioni 2.141 kwa mafungu yote matatu ambapo kati yake, zaidi ya  Sh trilioni  1.9 ni kwa matumizi ya kawaida na zaidi ya  Sh bilioni 164 kugharamia miradi ya maendeleo. 

Mchanganuo wa bajeti hiyo ni Ngome inaomba zaidi ya Sh  trilioni 1.617, JKT zaidi ya Sh  bilioni 354.234 na Wizara Sh bilioni  169.

VIPAUMBELE VYA WIZARA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Kazi na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama, akisoma hotuba ya wizara hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema mpango na mwelekeo wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika mwaka wa fedha 2020/21 ni kutekeleza majukumu yake kwa weledi kulingana na dira na dhima yake. 

Alisema mwelekeo wa kazi zinazokusudiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2020/21 utazingatia maeneo ya kipaumbele ambayo ni  kuliimarisha jeshi kwa zana na vifaa vya kisasa, mawasiliano pamoja na rasilimali watu.

Pia kuendelea kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Wanajeshi ikiwemo mafunzo, matunzo ya zana na miundombinu, maslahi, huduma bora za afya, ofisi na makazi.

Vilevile  kuendelea kujenga uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuboresha miundombinu ili liweze kuchukua vijana wengi zaidi na kutoa mafunzo ya uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa na stadi za kazi kwa vijana wa Kitanzania.

Pia kuendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia ili kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia.

Waziri huyo alisema kipaumbele kingine ni  kuendelea kuimarisha na kuratibu Jeshi la Akiba pamoja na kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya za Kikanda na nchi nyingine katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.

Pia  kuendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura inapohitajika na kuendelea kupima, kuthamini na kulipa fidia ya ardhi iliyotwaliwa kutoka kwa wananchi kwa matumizi ya jeshi.

HALI YA ULINZI

Waziri Jenista alisema katika mwaka wa fedha 2019/20, hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi  kwa ujumla imeendelea kuwa shwari na hapakuwa na matukio ya uhasama yaliyoripotiwa baina ya nchi  na nchi tunazopakana nazo. 

Alisema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeendelea kujizatiti ipasavyo kudhibiti ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu.

“Hata hivyo, zipo changamoto chache kwenye baadhi ya maeneo ya mipaka ya nchi zinazohitaji kutatuliwa ili udhibiti wa mipaka yetu uzidi kuimarika na kuimarisha usalama wa nchi yetu. Miongoni mwa changamoto hizo ni uharibifu wa alama za mipaka kwa baadhi ya maeneo ya mipaka,” alisema Jenista.

KAMATI YATAKA BAJETI ZAIDI JKT

Katika hatua nyingine, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, imeishauri Serikali iongeze bajeti ya vijana wanaotakiwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kuweka utaratibu utakaowawezesha vijana hao kupata ujuzi na uzoefu wa kazi za kujitegemea unaotambulika baada ya mafunzo yao.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo ya kamati hiyo bungeni jana,  Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Salum Mwinyi Rehani, alisema kamati hiyo inaiomba Serikali iongeze bajeti ya vijana wanaotakiwa kujiunga na JKT na kuweka utaratibu utakaowawezesha vijana hao kupata ujuzi na uzoefu wa kazi za kujitegemea unaotambulika baada ya mafunzo yao.

“Pamoja na kuongezeka bajeti ya wizara hii kwa mwaka wa Fedha wa 2020/2021, Serikali itoe kipaumbele kwa wizara hii wakati wa kutoa fedha hizo kwenye mafungu husika.

“Vilevile Serikali iyapatie fedha za kutosha mashirika ya Nyumbu na Mzinga ili yaweze kuendeleza tafiti zake zinazoendelea na kuanzisha tafiti mpya zenye tija kwa nchi yetu kwani dalili njema zimeanza kuonekana kama vile utengenezaji wa magari ya zimamoto.

“Pia kamati inatambua juhudi kubwa na kazi nzuri ya Serikali ya awamu ya tano katika ukusanyaji wa mapato, kutokana na ufanisi huo wa ukusanyaji wa mapato Serikali iongeza ukomo wa bajeti kwa mafungu yote ya wizara hiyo kwa kiwango cha kuweza kukabiliana na changamoto zenye umuhimu zaidi kutatuliwa katika Wizara hii,” alisema Rehani.

Alisema kamati inashauri Serikali itoe fedha zinazohitajika katika ujenzi wa makao makuu ya ulinzi – Kikombo, Dodoma ili ujenzi huo uendane na wakati na kuepukana na kufidia bajeti ya gharama zitakazozidi.

 “Serikali iipatie fedha wizara hii kwa ajili ya kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na yanayotarajiwa kuchukuliwa kwa ajili ya matumizi ya jeshi,” alisema Rehani.

Alisema kamati hiyo inaiomba  Serikali ione umuhimu wa kufanya ukarabati wa haraka wa nyumba za makaazi ya wanajeshi kwa kuanzia na zile ambazo zipo katika hali isiyoridhisha ili kuepuka gharama kubwa inayoweza kujitokeza ya kuzijenga upya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles