26.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 24, 2021

BAJETI YA KILIMO PASUA KICHWA

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

WAKATI hali ya chakula ikiripotiwa kutokuwa nzuri nchini, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti yake, ikionyesha kupungua kwa Sh bilioni 7.198.

Bajeti hiyo, iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma jana, inaonyesha pia kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mpaka kufikia Mei, serikali ilikuwa imetoa asilimia 3.31 pekee ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge mwaka jana kwa ajili ya sekta ya kilimo.

Hali ilivyo

Akiwasilisha bajeti yake, Dk. Tizeba alisema kwa mwaka wa fedha 2017/18,  wizara yake inaomba kuidhinishiwa Sh bilioni 267.865.

“Katika fungu 43 (kilimo) jumla ya Sh bilioni 214.815 zinaombwa. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 64.562 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 150.253 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Katika fungu 99 (mifugo), jumla ya Sh bilioni 29.963 zinaombwa, zikiwamo Sh bilioni nne za maendeleo na Sh bilioni 25.963 za matumizi ya kawaida.

“Fungu 64 limeombewa Sh bilioni 16.792 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni mbili ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Kwa upande wa fungu 24 (ushirika), Sh bilioni 6.293 zinaombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Katika mwaka wa fedha 2016/17, bajeti iliyopitishwa na Bunge ilikuwa Sh bilioni 275.063.

Katika bajeti hiyo, fungu 43 (kilimo) lilitengewa Sh bilioni 210.359, zikiwamo Sh bilioni 109.831 za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 100.527 za maendeleo.

“Hadi kufikia Mei mwaka huu, Sh bilioni 61.702 zilikuwa zimetolewa ambazo ni sawa na asilimia 54.52 ya fedha zilizokuwa zimeidhinishwa kwa ajili ya matumizi mengineyo.

“Kupitia fungu hilo la 43, kwa upande wa shughuli za maendeleo, wizara ilitengewa Sh bilioni 100.527. Aidha, wizara ilipokea fedha kwa ajili ya kulipia madeni ya makandarasi wa skimu za umwagiliaji na kufanya fedha zilizoidhinishwa kuongezeka hadi kufikia Sh bilioni 101.527.

“Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 23 ni fedha za ndani na Sh bilioni 78.527 ni za nje. Hadi kufikia Mei 4, mwaka huu, Sh bilioni 3.369 zilikuwa zimetolewa, ambazo ni sawa na asilimia 3.31 ya fedha zilizoidhinishwa,” alisema Dk. Tizeba.

Athari za ukame

Akizungumzia ukame uliotokea mwaka 2016/17, Dk. Tizeba alisema ulisababisha vifo vya mifugo katika mikoa tisa ya Dodoma, Pwani, Morogoro, Singida, Manyara, Shinyanga, Mara, Arusha na Kagera.

Aliitaja idadi ya ng’ombe waliofariki katika mikoa hiyo, kuwa ni 102,987, mbuzi, 14,881, kondoo 13,815 na punda 646.

Kuhusu sekta ya uvuvi, alisema Serikali kupitia Mamlaka ya kusimamia uvuvi katika bahari kuu, imefanya mabadiliko katika kanuni zake ambapo meli za kigeni zinazokata leseni za uvuvi zitatakiwa kuajiri vijana wa Kitanzania ili wafanye kazi katika meli hizo.

Serikali itakachofanya

Dk. Tizeba pia alisema, Serikali imefuta kodi, tozo na ada 108 walizokuwa wakitozwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.

Alisema Serikali imelazimika kuchukua hatua hiyo kwa kuwa, kodi, tozo na ada hizo zilikuwa kero katika sekta hizo.

“Katika mwaka 2017/18, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kodi, tozo na ada ambazo ni kero kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, zinafutwa na kubaki zile zenye uhusiano wa moja kwa moja na sekta husika.

“Kwenye sekta ndogo ya mazao, katika mwaka 2017/18, Serikali itafuta jumla ya tozo 80 kati ya tozo 139 zinazoonekana kuwa kero kwa wakulima na pia itapunguza viwango vya tozo nne, zilizopo,” alisema Dk. Tizeba.

Aliyataja maeneo yaliyofutiwa, kodi, tozo na ada hizo katika sekta ya kilimo kuwa ni kahawa, tumbaku, sukari, pamba, korosho na katika zao la chai.

“Pamoja na hayo, Serikali itaendelea kuchambua kwa kina tozo, ushuru na ada mbalimbali zilizobaki katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuangalia uhalali wa kuwapo kwake,” alisema Dk. Tizeba.

Wakati huo huo, Dk. Tizeba alisema kuanzia Julai mwaka huu, Serikali itasitisha uchinjaji wa punda ili kuokoa wanyama hao wasitoweke nchini.

“Serikali itasitisha uchinjaji wa punda wanaokadiriwa kuwa 500,000 kuanzia Julai mosi mwaka huu, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu au kumalizika kwa wanyama hao kwa kuwa wanachinjwa kwa kasi.

JWTZ wakabili uvuvi haramu

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imeitaka Serikali kuongeza nguvu ili kukabiliana na uvuvi haramu nchini kwa kuwatumia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Mary Nagu, akisoma maoni ya kamati yake, alisema: “Pamoja na wizara kupitia Idara ya maendeleo ya uvuvi kuendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu ambavyo bado vinaendelea kushamiri mahali pengi nchini, bado vitendo hivyo vinaendelea kutokea.

“Kwa hiyo, kamati inashauri Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kukabiliana na uvuvi haramu, ikiwa ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya doria kwenye maeneo ya maziwa, ikiwa ni pamoja na kushirikisha Jeshi la Wananchi katika kufanya doria ili kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu,” alisema Dk. Nagu.

Katika hatua nyingine, alisema kuna haja Serikali kuwa na kanda maalumu ya kilimo cha umwagiliaji ili iweze kusaidia katika kuinua kilimo nchini.

Upinzani wataka sheria zibadilishwe

Naye Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wizara hiyo, Secilia Pareso, alisema kuna haja Serikali kuangalia sheria zake ili nyavu zinazotumika kuvulia samaki katika Ziwa Tanganyika, zitofautiane na zinazotumika katika Ziwa Victoria kwa kuwa baadhi ya samaki wanatofautiana ukubwa, hasa dagaa.

Pamoja na hayo, alitaka kujua Serikali itachukua hatua gani za kuwafidia wafugaji ambao mifugo yao ilikufa kutokana na ukame katika mwaka 2016/17.

 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,967FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles