26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

BAJETI KILIMO KAA LA MOTO


Na MAREGESI PAUL - DODOMA    |

BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na wale wa upinzani, wameendelea kuionyesha kidole Wizara ya Kilimo, wakionyesha kutoridhishwa na fedha ilizotengewa kwenye bajeti ya sekta hiyo kwa mwaka 2018/19, na mipango yake ya kukwamua wakulima nchini.

Wizara hiyo iliwasilisha bajeti yake juzi bungeni, ikiomba kuidhinishiwa Sh bilioni 170.2 kwa mwaka 2018/19, ikiwa ni pungufu kwa asilimia 23, ikilinganishwa na ya mwaka 2017/18 iliyokuwa Sh bilioni 221.

Sehemu kubwa ya wabunge waliochangia bajeti hiyo juzi na jana, walionyesha kutoridhishwa nayo, huku wengi wakishawishi wenzao kutoipitisha ili Serikali ijipange upya, wakidai sekta hiyo ndiyo inayotegemewa na sehemu kubwa ya Watanzania.

NAPE NNAUYE

Akichangia, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, alisema kuna kila sababu bajeti hiyo kuondolewa bungeni kwa kuwa idadi kubwa ya wabunge walioichangia hawaiungi mkono.

“Katika michango ya wabunge wa pande zote mbili, wengi wao hawaungi mkono bajeti hii.

“Kama ni suala la maendeleo ya watu, bajeti hii ndiyo inagusa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania na kelele tunazosikia kwenye pamba na kwenye mazao mengine, ni kwa sababu sekta hii inagusa maisha ya watu moja kwa moja.

“Lakini, bado tunayo nafasi ya ujumbe tunaotaka kuupeleka kwenye umma, kwamba tunajali nini kati ya maendeleo ya vitu au maendeleo ya watu ambao ndio waliotuweka madarakani.

“Ukiangalia ‘trendi’ ya mwaka 2016/17, utaona Serikali ilitenga asilimia 0.93 kwenye bajeti kwa ajili ya Wizara ya Kilimo, bajeti ya mwaka 2017/18 ikashuka hadi asilimia 0.85 na katika mapendekezo ya sasa hivi, tumeshuka tena hadi kwenye asilimia 0.52 ya bajeti yote.

“Hii maana yake ni kwamba kila mwaka tunashusha bajeti tunayotenga kwenye sekta inayogusa watu zaidi ya asilimia 80 kuliko sekta nyingine.

“Kwahiyo, ushauri wangu katika hili, Serikali isione aibu kuipitia upya bajeti hii kwani tukiipitisha kama ilivyo, ujumbe kwa Watanzania ni mbaya sana kwa Serikali ya awamu ya tano na itaonyesha tunataka kuwekeza zaidi kwenye vitu badala ya watu.

“Nikiikubali bajeti hii, wananchi wa korosho, mbaazi, ufuta, pamba na wengineo watanishangaa.

“Pamoja na hayo, naangalia ilani ya CCM ambayo baadhi yetu hawataki tuinukuu, naona inapingana na bajeti hii. Kwahiyo, tuishauri Serikali irudi mezani, iende ikaipitie upya na kuweka vipaumbele vya wananchi,” alisema Nape.

Pamoja na hayo, Nape alihoji ni mahali gani zinakokwenda fedha pindi Serikali inapobana matumizi na pia fedha hizo zinakwenda wapi kila Serikali inapoongeza makusanyo ya mapato.

Katika mchango wake huo, Nape alionyesha kutoridhishwa na vipaumbele vya Serikali kwa kile alichosema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika miradi mikubwa inayoweza kujiendesha yenyewe na kushindwa kuwekeza fedha za kutosha katika miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

HUSSEIN BASHE

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, aliungana na Nape na kutaka bajeti hiyo iondolewe bungeni kupitia kanuni ya 69 ili Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha, wakakae na kuona jinsi ya kuiboresha.

“Sisi wabunge hasa wa Chama Cha Mapinduzi, tuna wajibu wa kuwalinda wakulima wakiwamo wa mahindi, pamba, wafugaji wa ng’ombe na wavuvi wa samaki, lakini sisi ndio tunaowanyanyasa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu amempa binadamu utu na akili ya kuwajali wenzake, lakini sisi tunawanyanyasa wenzetu.

“Kwakuwa bajeti hii imetengewa fedha kidogo, nashauri tuirudishe ili ikaandaliwe upya,” alisema Bashe.

Katika maelezo yake, mbunge huyo alieleza jinsi wakulima wanavyotumia gharama kubwa katika kilimo na jinsi wanavyopata fedha kidogo wakati wa mauzo.

HILALLY AESHI

Naye Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Hilally Aeshi, aliungana na wabunge wenzake hao na kusema kuna haja bajeti hiyo ikaandaliwa upya na kuwasilishwa tena bungeni kwa kuwa Bunge bado lina muda wa kutosha.

Pamoja na hayo, alitaka wakulima waruhusiwe kuuza mazao yao popote wanapotaka na pia Serikali ilipe madeni ya mawakala wa pembejeo za kilimo kwa kuwa baadhi yao wameanza kupoteza maisha kutokana na madeni wanayodaiwa.

MARIAM DITOPILE

Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Ditopile, alianza kwa kusema Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim majaliwa, wana dhamira ya dhati kuwasaidia Watanzania na ndiyo maana kwenye ziara zao zote lazima watatue matatizo ya wakulima.

Pia alisema, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, ni rafiki yake, lakini urafiki huo haujazidi alionao na wakulima.

“Dk. Tizeba wewe ni shwahiba wangu, lakini ushwahiba huo si kama nilionao kwa wakulima wa nchi, najua jasho wanalolitoa, najua jinsi gani wanavyojikwamua na mazingira magumu, lakini wanataka kuipatia nchi yetu kipato kikubwa, kwahiyo leo hii nasimama kwa niaba ya wakulima wangu, naomba niseme machungu wanayopata, tena nasema kwa takwimu.

“Nianze na zao la mahindi, Tanzania ilishatoka kwa kilimo cha chakula, hatulimi mahindi kwa chakula, tunalima kwa biashara na chakula, leo hii ripoti yake mwenyewe inamsuta, hapa anasema tumezalisha zaidi ya asilimia 120, kwahiyo suala lako la kusema tulinde ‘food security’ tusiwaumize watu tunaowaambia walime kwa biashara.

“Mimi mwenyewe ni kijana ambaye ni mkulima, nina mwaka wa saba kwenye kilimo, lakini nasikitika kusema ni mwaka wa kwanza (mwaka huu) sijalima, juzi nimetoka kutupa gunia 6,500 zimeoza, tunaelekea wapi?

“Hivi mheshimiwa Tizeba, unaenda kuwashauri viongozi wetu wakuu unawalisha matango pori kwanini? Leo hii tayari tuna ziada ya mahindi, unaenda kuweka zuio la kuuza mahindi nje, lakini unaruhusu mahindi yaingie, basi siungeacha tuminyane wenyewe ndani?” alihoji Ditopile.

Alisema kilimo ni kigumu, mkulima hapati mbegu wala kitu chochote kutoka serikalini, lakini waziri anajibu kirahisi tu kwamba ni wachuuzi ndio wanapiga kelele.

“Kwani wachuuzi wanaenda kununua na mawe yale mahindi?” alihoji.

Alisema ni bora Serikali ingekataza mahindi yasitoke nje na pia isiruhusu yanayotoka nje ya nchi kwani sasa hivi Zambia wameingiza mahindi, Mtwara, Lindi na hadi Himo yapo.

Ditopile pia alisema; “kitendo cha Serikali kuruhusu mazao kama korosho yalimwe nchi nzima ni cha ajabu kwa sababu mmeleta miche Dodoma na kuigawa kwa wananchi na sasa imekauka kwa sababu hamkuwaandaa na hakuna hata maofisa ugani.

“Kwahiyo, mheshimiwa waziri, nakwambia kama asilimia kumi ya miche ya korosho iliyopandwa mkoani Dodoma itaota, nitajiuzulu ubunge.”

Pamoja na hayo, mbunge huyo alimshutumu Dk. Tizeba na kusema amechangia kuua kilimo cha tumbaku na mahindi nchini ingawa ameaminiwa na Rais.

ANDREW CHENGE

Wakati hao wakisema hayo, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, alipinga bajeti hiyo kuondolewa bungeni na badala yake akataka ipitishwe kisha itumike kanuni ya Bunge ya 105 kujadili maeneo yaliyolalamikiwa kabla ya bajeti kuu kuwasilishwa.

Pamoja na hayo, alipinga utaratibu wa Serikali wa kutumia vyama vya ushirika kununua mazao na badala yake akataka utumike utaratibu mwingine.

WABUNGE WA UPINZANI

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Willy Qambalo (Chadema), alisema Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, hatofautiani na waziri kivuli ambaye huwa hana fedha za kuendeshea wizara.

PAULINE GEKUL

Naye Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), alisema Serikali haiwezi kufanikiwa katika suala la viwanda kwa sababu imeshindwa kuimarisha sekta ya kilimo.

ABDALLAH MTOLEA

Akichangia bajeti hiyo, wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), alisema wakati Tanzania inatenga Sh bilioni 170 kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Rwanda wanatenga Sh bilioni 8.

Kutokana na hali hiyo, alisema sera ya Tanzania ya viwanda haitawezekana kama Serikali haitaongeza fedha katika sekta ya kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles