Na FREDY AZZAH-DODOMA
NI bajeti ya mkakati. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2017/18 ya Sh trilioni 31.712.
Bajeti hiyo imetoa nafuu ya kodi kwa wananchi wa kawaida na kuongeza kwa wale wa kipato cha kati na baadhi ya kodi zikifutwa zikiwamo za mazao ya kilimo na mifugo, huku vinywaji baridi, vikali, pombe, uchakavu wa magari na mafuta ya petroli zikipanda.
Pamoja na mambo mengine, Serikali imeanzisha vyanzo vingine vya kodi vilivyoonekana kuwa ni tata kukusanywa, ikiwa ni pamoja na kodi ya nyumba. Kwa sasa, nyumba za kawaida zisizothaminishwa zitalipa Sh 10,000 huku zile za ghorofa zikilipiwa Sh 50,000 kwa kila ghorofa kwa mwaka.
MFUMO WA KODI
Akiwasilisha bajeti hiyo jana, baada ya Bunge kujadili bajeti za kisekta kwa wiki tisa, Dk. Mpango alisema Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mtaji ili kupunguza gharama za ununuzi, uagizaji wa mashine na mitambo ya kuzalishia na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.
Alisema hatua hiyo itahusisha viwanda vya mafuta ya kula, nguo, ngozi, madawa ya binadamu na mifugo.
“Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo cha mazao na mifugo, na kukuza ajira na uchumi wa nchi.
“Aidha, hatua hii itawezesha viwanda vidogo na vya kati kupata unafuu wa gharama za kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mashine na mitambo watakayonunua kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
“Mitambo na mashine zote zitakazosamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani zitaainishwa kwa kutumia HS Codes,” alisema Dk. Mpango.
Alisema Serikali inafuta Kodi ya Ongezeko la Thamani katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa na mizigo nje ya nchi.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu kwa kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine, hususan zisizo na bandari.
“Hatua hii itahamasisha wasafirishaji kutoka nchi jirani kupitisha mizigo yao kwa wingi kwenye bandari zetu na hivyo kukuza uchumi wa nchi kutokana na kuongezeka kwa mapato ya bandari. Vile vile kukua kwa sekta ya bandari kutachangia kuongezeka kwa ajira nchini,” alisema.
Alisema kodi hiyo iliyofutwa ilianzishwa kwenye bajeti inayofikia kikomo, ambayo licha ya kupigiwa kelele na wabunge wengi na wadau wa Serikali, Serikali ilisisitiza kuendelea kuitoza.
Dk. Mpango alisema pia Serikali inakusudia kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyakula vya mifugo vinavyotengenezwa nchini, vinavyotambulika kwenye HS Code 2309.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za kununua vyakula hivyo kwa wafugaji,” alisema.
Alisema Serikali pia inasamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mashine ya mayai ya kutotolesha vifaranga, lengo likiwa ni kupunguza gharama za uzalishaji wa vifaranga na kukuza sekta ndogo ya ufugaji ili iweze kuongeza mchango wake katika pato la taifa.
“Hatua hizi zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 48.034,” alisema.
Dk. Mpango alisema Serikali pia inafanya marekebisho ya sheria ya kodi ili kurekebisha muda uliotolewa katika kutoza kodi mbadala kwa kampuni zinazopata hasara kwa miaka mitatu mfululizo badala ya miaka mitano mfululizo.
“Lengo la hatua hii ni kuoanisha na aya ya nne ya kifungu cha nne cha sheria hiyo, kinachotamka kwamba kodi hiyo inatozwa kwa miaka mitatu mfululizo,” alisema Dk. Mpango.
Alisema Serikali pia inaongeza kiwango cha juu kinachotumika kukokotoa uchakavu wa magari yasiyo ya kibiashara kutoka Sh milioni 15 hadi Sh milioni 30.
“Lengo la hatua hii ni kufanya gharama za magari hayo ziendane na gharama halisi za soko.
“Marekebisho haya yamezingatia kwamba kiwango cha sasa cha Sh milioni 15 ni cha muda mrefu na hakiakisi bei halisi ya magari kwa sasa katika soko,” alisema.
Kodi nyingine iliyofanyiwa marekebisho ni ya Mapato ya Makampuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 kwa miaka mitano kuanzia mwaka mwekezaji atakapoanza uzalishaji, kwa waunganishaji wa magari, matrekta na boti za uvuvi.
“Lengo la hatua hii ni kuongeza ajira, kuongeza mapato ya Serikali na pia kuhamasisha uhaulishaji wa teknolojia. Aidha Serikali itaingia mkataba wa makubaliano na utekelezaji (Performance Agreement) na kila muunganishaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande,” alisema.
Alisema Serikali pia itaanza kutoza Kodi ya Zuio kwa asilimia 5 kwenye bei ya kuuzia (total market value) ambayo itakua ni kodi ya zuio ya mwisho (final Withholding Tax) kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya aina zote.
Alisema hatua hizo zitaongeza mapato ya Serikali kwa Sh milioni 88.5.
USHURU WA VINYWAJI
Kwa upande wa ushuru wa vinywaji, alisema kwenye vinywaji baridi ushuru unapanda kutoka Sh 58 kwa lita hadi Sh 61 kwa lita, maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka nje, kutoka Sh 58 kwa lita hadi Sh 61, ushuru wa maji yanayozalishwa nchini utabaki kuwa Sh 58 kwa lita.
Kwa upande wa ushuru wa maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini utashuka kutoka Sh 9.5 kwa lita hadi Sh 9.0, maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi nchini ushuru utapanda kutoka Sh 210 kwa lita hadi Sh 221.
Ushuru wa bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa utatoka Sh 429 kwa lita hadi Sh 450, bia nyingine zote kutoka Sh 729 kwa lita hadi Sh 765.
Kwa upande wa ushuru wa bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka Sh 534 kwa lita hadi Sh 561, mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, utashuka kutoka Sh 202 kwa lita na kuwa Sh 200.
Kwa ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kodi inatoka Sh 2,236 kwa lita hadi Sh 2,349, vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje kutoka Sh 3,315 kwa lita hadi Sh 3,481, vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini itabaki kuwa Sh 3,315 kwa lita.
SIGARA JUU
Alisema ushuru wa sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, ushuru utatoka sh 11,854 hadi Sh 12,447 kwa kila sigara elfu moja, sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka Sh 28,024 hadi Sh 29,425 kwa kila sigara elfu moja.
Dk. Mpango alisema ushuru wa sigara zenye sifa nyingine unatoka Sh 50,700 hadi Sh 53,235 kwa kila sigara 1,000 huku tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara, ushuru wake ukitoka Sh 25,608 hadi Sh 26,888 kwa kilo na ule wa cigar ukibaki kuwa asilimia 30.
WENYE MAGARI KICHEKO
Alisema Serikali inadhamiria kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari iliyokuwa inalipwa hata kwa magari ambayo hayatumiki ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu.
“Kufuta ada ya mwaka ya leseni ya magari ili ada hii ilipwe mara moja tu gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee kulipwa kupitia ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya petroli na dizeli kwa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya petroli.
“Dizeli na mafuta ya taa kama ilivyoainishwa katika aya ya 69(ii). Serikali inatoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada hiyo yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma,” alisema Dk. Mpango huku wabunge wakilipuka kwa furaha.
Alisema badala yake ada hiyo itatozwa kwa magari yanayotembea tu. Kwa sababu hiyo, ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na taa utaongezeka kwa kiasi cha Sh 40 kwa lita moja kutoka Sh 339 kwa lita hadi Sh 379.
Kwa mafuta ya dizeli, alisema ushuru wake utatoa Sh 215 kwa lita hadi Sh 255 na mafuta ya taa yakitoka Sh 425 kwa lita hadi Sh 465.
“Hatua za ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 27.801,” alisema.
Alisema pia Serikali inapendekeza kuongeza ada ya leseni ya magari wakati wa usajili mara ya kwanza.
Waziri Mpango alisema gari lenye ujazo wa injini ya 501-1500 cc ada itaongezeka kutoka kiwango cha sasa cha Sh 150,000 hadi Sh 200,000, ikiwa ni ongezeko la Sh 50,000.
Alisema gari lenye ujazo wa injini ya 1501-2500 cc kutoka kiwango cha sasa cha Sh 200,000 hadi Sh 250,000, ikiwa ni ongezeko la Sh 50,000.
Lenye ujazo wa injini ya 2501 cc na zaidi kutoka kiwango cha sasa cha Sh 250,000 hadi Sh 300,000, ikiwa ni ongezeko la Sh 50,000.
“Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 77.603,” alisema.
Kuhusu Serikali za mitaa, alisema anafanya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 ili kupunguza ushuru wa mazao unaotozwa na halmashauri za wilaya kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 ya thamani ya mauzo hadi asilimia 3 kwa mazao ya biashara na asilimia 2 kwa mazao ya chakula.
“Mtu anayesafirisha mazao yake kutoka halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani moja (1) asitozwe ushuru. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wakulima kulipwa bei stahiki ya mazao yao na hivyo kuboresha mapato yao. Hatua hii inatarajiwa kuhamasisha uzalishaji wa mazao,” alisema.
Alisema Serikali pia inafuta ada ya ukaguzi wa viwango, ada ya ukaguzi wa mionzi na ada ya wakala wa vipimo kwenye mbolea inayotozwa na Shirika la Viwango Tanzania, Tume ya Mionzi Tanzania na Wakala wa Vipimo Tanzania, lengo likiwa ni kuwapunguzia wakulima gharama za pembejeo na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji.
Waziri Mpango alisema Serikali inafuta ada ya ukaguzi wa viwango kwa mazao ya biashara kama pamba, chai, korosho na kahawa inayotozwa na Shirika la Viwango Tanzania na lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa viwanda vinavyosindika mazao haya na pia kuongeza mapato kwa wakulima.
NYUMBA ZA KULALA WAGENI
Alisema Serikali inapendekeza kufuta ushuru wa huduma (Service Levy) kwenye nyumba za kulala wageni ambazo zinatozwa Guest House Levy.
“Kufuta ushuru wa mabango kwa mabango yanayoelekeza mahali huduma za jamii (Shule na Hospitali au Zahanati) zinapopatikana. Aidha kuanzia Julai Mosi, mwaka huu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaanza kukusanya ushuru wa mabango ya matangazo kwa nchi nzima.
“Kufuta ada ya vibali vinavyotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa mfano vibali vya machinjio (isipokuwa ada ya machinjio na ada ya ukaguzi wa nyama), ada ya vibali vya kusafirisha mifugo na ada ya vibali vya kuanzisha maduka ya dawa.
“Kufuta ada ya makanyagio minadani na kufanya marekebisho ya kiwango cha faini kwa makosa ya watakaoenda kinyume na masharti ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa kutoka kiasi kisichozidi Sh 50,000 na kifungo kisichozidi miezi 12 hadi kiasi kisichopungua Sh 200,000 na kisichozidi Sh 1,000,000 au kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miaka miwili,” alisema.