BABA WATATU WANAOSHINDANA KUZAA KUIJAZA DUNIA

0
594

WANAUME watatu wakiwamo mtu na kaka yake, kwa pamoja wamezaa watoto karibu 100 huku ndoto yao ilikuwa ni kufikisha watoto 300.

Watatu hao ni kielelezo cha kupaa kwa kasi kwa idadi ya watu nchini Pakistan, huku watu wakihesabiwa kwa mara ya kwanza kipindi cha miaka 19.

Lakini katika taifa ambalo wataalamu wanaonya  kuwa kupaa kwa idadi ya watu kusikoendana na mafanikio ya kiuchumi na kijamii, watatu hao hawaonekani kuwa na wasiwasi, wakisema Mungu daima ni mpaji.

Pakistan ina kiwango cha juu cha uzazi barani Asia, ikiwa na wastani wa watoto watatu kwa kila mwanamke, kwa mujibu wa takwimu za serikali na Benki ya Dunia na sensa iliyofanyika mwaka huu inataarajia kuonesha ukuaji wa juu zaidi.

“Mungu aliumba ulimwengu mzima na wanadamu wote, hivyo kwanini nisitishe mchakato asilia wa uzaaji watoto?” alihoji Gulzar Khan, baba wa watoto 36, akigusia moja ya Imani kubwa katika eneo hilo: Ni kwamba Uislamu unazuia uzazi wa mpango.

Uadui wa kikabila ni sababu nyingine eneo hilo la kaskazini magharibi mwa nchi, ambako mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 57 anaishi katika Jiji la Bannu na mke wake wa tatu, ambaye kwa sasa ana mimba.

“Tunataka kuwa na nguvu,” alisema huku akiwa amezungukwa na watoto wake 23. Ni wengi na hawahitaji marafiki wa kucheza nao bali hucheza wao kwa wao,” anasema katika hali ya kujivunia na kujiamini.

Ndoa za mitaala ni halali lakini zilizo nadra nchini Pakistan na familia kama za Khan si mila na desturi yao ijapokuwa imani hiyo imeenea zaidi wanapoishi.

Sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 1998, ilionesha Pakistan ina idadi ya watu wanaofikia milioni 135 na sensa mpya iliyofanyika mapema mwaka huu ambayo matokeo ya awali yanatarajia kutangazwa mwezi ujao inabashiri idadi hiyo itafika milioni 200.

Uchumi unakua kwa kasi kuliko ilivyokuwa mwongo uliopita na mwezi uliopita Serikali ya Islamabad ilipaisha bajeti yake ya maendeleo hadi asilimia 40. Lakini wachambuzi wanaonya idadi ya watu itakwamisha maendeleo hayo yaliyofikiwa, ikitumia rasilimali zilizopo katika taifa la vijana ambao upatikanaji wa ajira kwa ajili yao ni adimu na karibu watu milioni 60 wanaishi chini ya mstari wa umasikini.

“Ni wazi hilo ni tatizo kwa sababu linaathiri mafanikio ya sekta ya afya vibaya, pia kutafuna mafanikio mengine ya kimaendeleo,” anasema Zeba Sathar, Mkurugenzi wa Baraza la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa.

Sathar alitabiri kuwa sensa itaonesha ukuaji umepungua kutokana na kiwango cha chini cha utungaji mimba, ijapokuwa aliongeza kuwa kitabakia juu katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa nchi.

Kaka wa Khan, Mastan Khan Wazir — mmoja wa watoto wake 15 pia ana wake watatu hadi sasa, Wazir amezaa watoto 22 tu, lakini kama ndugu yake anasema wajukuu wake wako wengi mno.

Mzee huyo wa miaka 70 mwenye sharubu nzito ni nyota fulani mdogo katika wilaya iliyotopea kwa ukabila ya North Waziristan.

“Mungu aliahidi kwamba atatupatia chakula na rasilimali lakini watu wana imani dhaifu,” alisema akiwa amevalia vazi rasmi la wenyeji wa Waziristani.

Katika jiji la kusini magharibi la Quetta katika Jimbo la Balochistan, Jan Mohammed, baba wa watoto 38 anakubaliana na imani zinazoshikiliwa na wenzake hao wawili licha ya kwamba huko nyuma aliwahi kuiomba serikali iisaidie famiia yake.

Jan anakumbukwa mwaka 2016 aliposema ndoto na matamanio yake ni kuongeza mke wa nne katika harakati zake za kuelekea kupata watoto 100.

Hata hivyo, hakuna mwanamke aliyekubali mitala hiyo bado, lakini anasema na kusisitiza kwamba hajakata tamaa kufanikisha azma yake hiyo.

“Kwa kadiri idadi ya Waislamu inavyoongezeka, ndivyo maadui wetu watakavyowaogopa kwa wingi wetu. Waislamu wanapaswa kuzaa watoto zaidi na zaidi,” anasema.

Wakiwa wamezuiwa na waume zao kuzungumza, hakuna mmoja wa wake watatu wa wanaume hao mwenye ubavu wa kutoa ushauri au maoni yao kuhusu uzazi wa mpango katika Uislamu.

Lakini tayari kuna mwamko mkubwa nchini Pakistan kuhusu hitaji la uzazi usio holela au kuruhusu mwili wa mwanamke kupumzika angalau miezi 18 baina ya mimba, Sathar alisema.

“Hitaji la taarifa za wazi kuhusu njia za uzazi wa mpango zinapatikana, namna zinavyofanya kazi, uwezekano wao na wapi pa kuzipata. Hilo linakosekana,” aliongeza.

Kuwapatia wanawake uchaguzi wa kuamua au kushauri kunaweza kusaidia, anasema Aisha Sarwari, mwanaharakati wa masuala ya wanawake ambaye aliwahi kuandika ukuaji wa idadi ya watu na haki za wanawake.

Khan, mwishowe amekiri kunaweza kuwa na manufaa ya upunguzaji kasi ya uzao.

Kwa kitu kimoja kilichomfanya aamini hivyo ni kupungua uadui kaskazini magharibi mwa nchi katika miaka ya karibuni.

Anasema; “sasa kwa neema ya Mungu, hali imebadilika — vita na mapigano vimemelizika — hivyo, sasa kupunguza idadi ya watu si mbaya.”

Hilo litamfanya pia ajikite kwa shughuli nyingine anasema na kuongeza: “Iwapo mtu ana watoto wachache, hulazimika kufanya sana tendo la ndoa na wake zake.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here