Derick Milton -Simiyu
IKIWA ni takribani mwezi mmoja tangu Januari 9, Baraza la Mitihani (NECTA), lilipotangaza matokeo ya kidato cha nne na Yohana Lameck (19) kuibuka shujaa wa shule za kata kwa ufaulu wa A tisa licha mazira magum aliyokuwa nayo, baba yake aliyeikimbia familia kwa miaka saba, ameibukia kwenye hafla ya kumpongeza.
Yohana aliyekuwa akisoma shule hiyo ya kata iliyopo wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, kwa miaka saba alikuwa akiishi na mama yake huku wakiwa na maisha magumu ambapo wakati mwingine, alilazimika kuacha shule na kufanya kazi za vibarua za kulima, kuchunga ngombe ama kusukuma mikokoteni ili aweze kupata chakula.
Walimu wake wa shule ya msingi, ndio waliompeleka shule ya sekondari baada ya kumuona mtaani licha ya kwamba amefaulu na alipokuwa sekondari, kuna wakati aliacha shule kwa miezi mitatu baada ya kukosa mahitaji muhimu ikabidi walimu wake wamsake na kumrudisha shuleni na kumpa mahitaji kama sare na chakula.
Katika shule aliyosoma Yohana wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 88 ambapo yeye pekee ndiye aliyepata daraja la kwanza.
Waliopata daraja la pili ni wanne, daraja la tatu 15, daraja la nne 54 na sifuri 13 huku shule yake ikishika nafasi ya 79 kati ya shule 100 kwenye mkoa na nafasi ya 1991 kati ya shule 3908 kitaifa.
Kwa mujibu wa matokeo hayo masomo aliyofanya Yohana na ufaulu wake kwenye mabano ni Civics (A) Historia (A), Jographia (A) Kiswahili (A) Kingereza (A) Phizikia (A) Kemia (A) Bayolojia (A) na Hisabati (A).
Baba aibuka
Juzi Mkoa wa Simiyu, ulifanya hafala ya kupongeza wanafunzi waliofaulu mtihani huo ambapo Lameck Lugedenga baba mzazi wa Yohana aliibuka na kufanya minong’ono kuibuka ukumbini.
Aliwasili ukumbini hapo akiwa ameambatana na mke wake Mariamu Lulyalya pamoja na Yohana.
Baada ya kutambulishwa kuwa ndiye baba mzazi wa Yohana, kulizuka gumzo na minong’ono ukumbini kwani taarifa za kutelekeza familia kwa miaka saba zilikuwa zinajulikana badaa ya kuandika na vyombo vya habari.
Lugedenga alimuacha Yohana akiwa darasa la nne Shule ya Msingi Igaganulwa, kutokana na umaskini na ilidaiwa alikimbilia mkoani Morogoro.
Akiongea na Mtanzania mara baada ya kumalizika kwa hafla hiyo, Lugedenga alisema ni kweli alikiimbia familia yake, kutokana na kuchanganyikiwa mara baada ya kifo cha mtoto wake wa kike Magreth aliyefariki dunia mwaka 2011.
Alisema Magreth alikuwa mmoja wa wanafunzi wenye uwezo mkubwa shuleni kumzidi Yohana, lakini baada ya kuugua kwa muda mfupi na kulazwa Hosptali ya Wilaya Bariadi (Somanda) alipoteza maisha.
“Marehemu alikuwa na uwezo mkubwa darasani, lakini alipoteza maisha zikiwa zimebaki siku mbili afanye mtihani wake wa kuhitimu darasa la saba, baada ya hapo nilichanganyika nikaamua kuondoka maana nilikata tamaa,” alisema Lugedenga.
Alisema mbali na hilo, ugumu wa maisha ulimfanya akate tamaa zaidi na kuamua kuondoka nyumbani kwake kwenda mkoani Morogoro kwa wazazi wake ambao walihamia huko muda mrefu.
“Niliunganisha vitu vyote hivyo nikaona niondoke, maana sina msaada na sina uwezo wa kuisadia familia yangu ni bora kuondoka nikatufute maisha sehemu nyingine,” alisema Lugedenga
Alisema mawasiliano na familia yake yalikuwepo ingawa kwa kiasi kidogo sana, kwani hata huko alipohamia hakuweza kufanikiwa kimaisha kutokana na kuendelea kupata matatizo ikiwemo kupoteza wazazi wake wote.
Aisema hakuwa na uwezo tena wa kuisadia familia yake na taarifa za mtoto wake Yohana kutaka kuacha shule alizipata, lakini alimsihi asiache bali awe mvumilivu kwani na yeye hana huwezo wa kumsaidia.
Aomba radhi
Lugedenga aliwaomba radhi mke wake na mtoto wake, kwa alichowafanyia na kusema hawezi kurudia tena na imekuwa fundisho kwake.
Alisema mtoto wake Yohana kufanya vizuri kwenye mtihani, kimefanya familia yake kuungana tena kwa mara nyingine na kamwe hawezi kurudia tena kuitelekeza.
“Nimejifunza siyo vizuri kuitelekeza familia hata kama ni shida, lazima uvumilie upambane nazo ukiwa na familia yako, nakiri nilikosena na ninashukuru mke wangu amenipokea tuendelee na maisha,” alisema Lugedenga.
Lugedenga alisema kwa kwa sasa hawezi tena kurudi Morogoro, bali ataanza maisha mapya na mke wake na mtoto wake licha ya kuwa hana uwezo atapamba kuhakikisha anahudumia familia yake.
“Nimekuja moja kwa moja siwezi tena kurudi Morogoro, bado maisha yangu ni magumu lakini nitapambana hivyo hivyo na mke wangu tuweze kuishi kama zamani,” alisema Lugedenga
Alisema kwa sasa anajisikia mwenye nguvu kutokana na alichokifanya mtoto wake, huku akiwashukuru walimu na wananchi ambao walimsaidia Yohana kupata mafanikio hayo.
Lugedenga alisema licha ya kuishi Morogoro kwa muda mrefu hajawahi kuwa na familia nyingine, bali alikuwa akiishi na wazazi wake na kujishughuliza na kilimo hivyo hana mke wala mtoto mwingine.
Mke anena
Mariamu Lulyalya alisema amemsamehe mme wake, kwani anajisikia mwenye furaha kuweza kuungana tena naye baada ya kuwakimbia kwa miaka saba.
Lulyalya anasema licha ya kutendewa mambo yote na mme wake, na kuachiwa mzigo wa kulea watoto, hawezi kumkataa kwani ndiye mme wake halali na wamefanikiwa kupata watoto watano.
“Leo najisikia mwenye nguvu sana, nashukuru mme wangu amerudi na tuko pamoja, alikuja nikampokea maana ni mme wangu na nimesamehe ili tuweze kuendeea na maisha,” alisema Lulyalya.
Yohana.
Yohana alisema kitendo cha baba yake kurudi nyumbani kumempa nguvu na anajisikia mwenye furaha kutokana na kukosa malezi yake kwa muda.
“Ni kweli mimi ni shujaa, bila mimi nahisi Baba asingerudi nyumbani, lakini kutokana na hiki ambacho nilikifanya leo amerudi, najisiki mwenye furaha sana, kama mtoto nilikuwa najisikia vibaya kukosa malezi ya baba,” alisema Yohana.
Mkuu wa Mkoa.
Awali Mkuu wa Mkoa huo, Antony Mtaka, alimtaka mzazi wa Yohana kuwa karibu na familia yake na kuhakikisha anamsaidia Yohana afike mbele zaidi ili aje kuwa msaada kwake.
Mtaka alimtaka Lugedenga kuhakikisha anashikamana na mtoto wake ikiwemo kuwasimamia wadogo zake kuhakikisha wanapata elimu, ili wawe msaada kwake na mke wake.
Akizungumzia matokeo ya kidato cha nne, Mtaka alisema mkoa kushika nafasi ya tano ndiyo lilikuwa lengo.
Aliwashukuru wadau wote wakiwemo wazazi, walimu na viongozi kwa kusaidia kufikia malengo hayo, huku akibainisha kuwa wataweka mikakati mipya kuhakikisha mkoa unashika nafasi tatu za juu.