27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Baba aua mtoto kwa mil. 5/-

ELIUD NGONDO, MBEYA

NI unyama.  Ndilo neno sahihi ambalo unaweza kusema, baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuwashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya mtoto, Rose Japhet (6), aliyeuawa Kijiji cha Msewe Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kutokana na imani za kishirikina.

Akizungumza na wandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei alisema watuhumiwa walimuua mtoto huyo Mei 3, mwaka huu kwa kumnyonga kisha kumnyofoa baadhi ya viungo.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Andrew Mwambuluma mkazi wa Mbalizi ambaye pia ni mmiliki wa shule ya Sekondari Ushindi na baba mzazi wa marehemu, Japhet Nguku (37) mkazi wa Kijiji cha Msewe wilayani Mbarali.

Kamanda Matei alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa umetelekezwa kwenye msitu wa Hifadhi wa Chimala wilayani Mbarali ukiwa umekatwa kanyagio la mguu wa kulia na baadaye ilibainika kuwa kanyagio hilo lilikuwa limefukiwa Mbalizi.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya fedha ambapo mzazi wa mtoto huyo, Japhet alikubali kumuuza mtoto wake kwa mmiliki wa shule ya Ushindi kwa shilingi milioni tano ili achukuliwe viungo na kwenda kutengeneza ndagu za biashara.

 “Japheti alikubali kumtoa mtoto wake kwa Andrew ambaye ni mfanyabiashara wa shule ya Sekondari ili akatwe kanyagio la mguu wa kulia kwa ajili ya kupeleka kwa mganga wa kienyeji ili atengenezewe ndagu (dawa ya utajiri) kwa ajili ya kuendeshea biashara,” alisema Kamanda Matei.

Alisema baada ya Japhet kukamatwa na kubanwa alieleza ukweli wa tukio hilo ambapo ilibainika kuwa kanyagio la mtoto huyo lilikuwa limewekwa kwenye karatasi ya plastiki, kisha kufukiwa Mbalizi umbali wa zaidi ya kilomita 70 kutoka eneo alipouawa.

 “Baada ya mmiliki wa shule kutajwa kuhusika na tukio hilo, alikamatwa na alipohojiwa alikiri kuhusika kisha wawili hao wakapelekwa mahabusu wakati uchunguzi unaendelea kufanyika ili kubaini ukweli zaidi,” alisisitiza Kamanda Matei.

Kamanda Matei alisema kwa sasa Jeshi hilo linaendelea na ufuatiliaji wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na msako wa kumtafuta mganga ambaye alikuwa anashirikiana na wauaji hao.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles