25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Baba amzuia mwanawe kufanya mtihani wa darasa la saba

mitihani-ya-darasa-la-saba-moro-3

NA WAANDISHI WETU, MKURANGA

MWANAFUNZI, Yusiria Msumi anayesoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Churwi katika Kijiji cha Mlamleni, Kata ya Tambani wilayani Mkuranga, amezuiliwa na baba yake mzazi kufanya mitihani ya taifa iliyoanza jana, bila sababu za msingi.

Inadaiwa mzazi huyo alimkataza mwanawe kufanya mitihani mwaka huu ili aufanye mwakani bila kuainisha sababu za uamuzi huo.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini,  baada ya mwanafunzi huyo kutofika shuleni jana,  Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo alitaka kujua sababu ya kutofanya mitihani hiyo.

“Leo (jana) asubuhi baada ya kukosekana kwa mwanafunzi huyo shuleni, Mwenyekiti alikwenda kumtafuta nyumbani kwao ambako alikuta mlango umefungwa.

“Akiwa njiani alikutana na wadogo zake na binti huyo ambao walimwambia kuwa dada yao kaenda shuleni,” alisema.

Alisema baada ya kuwabana wadogo zake walisema kuwa baba yao aliwaambia kuwa wakiulizwa waseme dada yao alikuwa anaumwa tumbo.

Shuhuda huyo alisema baba wa mwanafunzi huyo alikamatwa karibu na ofisi za serikali ya mtaa wa Churwi akijaribu kutoroka.

“Baada ya kukamatwa na kuhojiwa baba mzazi aliwapeleka katika vichaka ambako binti huyo alilikuwa amejificha na ndipo walipomrudisha na kumpeleka katika chumba cha mtihani,” alisema.

Alipoulizwa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani (RPC), Boniventure Mushongi,  alisema alikuwa katika msafara wa Makamu wa Rais hivyo atafutwe Kamanda wa Polisi Wilaya ya Mkuranga.

Kamanda wa Polisi Wilaya ya Mkuranga, Edson Kasekwa, alisema hakuwa na taarifa za kukamatwa   mtuhumiwa wa aina hiyo.

“Taarifa hizo sina kwa sasa nitaendelea kuzifuatilia huenda bado hawajamfikisha hapa, nitakapopata taarifa yoyote nitakujulisha,” alisema.

Mmoja wa walimu katika shule hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema mwanafunzi huyo amekuwa akishika nafasi ya kwanza darasani.

“Katika mitihani ya kufunga muhula aliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza darasani na katika mitihani ya kata aliongoza katika somo la hesabu,” alisema mwalimu huyo.

Habari hii imeandaliwa na Tunu Nassor, Paulina Kebaki(TUDARCO) na Teophil Mbunda(EHICO)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,606FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles