27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Baba ampeleka mwanawe shule, atembea kilomita 28

NI jambo la kawaida kwa baadhi ya wazazi katika maeneo mengi duniani kuwanyanyapaa na kuwatenga watoto wao wenye ulemavu ikiwamo kuwanyima haki zao za msingi.

Wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kuwaficha watoto wao kwa kuona aibu, vitendo vinavyofanywa zaidi na kina baba ambao huwakana na kuwatelekeza wake zao wanapozaa watoto wa aina hiyo.

Baadhi yao wamewaacha kwa ndugu na jamaa zao ambao wamekuwa wakiwafanyisha kazi nyingi za nyumbani na kuwakosesha kwa makusudi fursa za kielimu.

Ni tabia ambayo bado ipo hadi leo hii, licha ya kuwapo mikataba na matamko ya kimataifa kuhusu sheria na haki za wenye ulemavu, ambazo zimepitishwa katika nchi nyingi.

Hata hivyo, kuna wazazi wenye mapenzi mema kwa watoto wao wenye ulemavu wa aina hiyo kama baba huyu wa nchini China, Yu Xukang.

Yu badala ya yeye kuwa wa kwanza kumkana mwanawe na kumtelekeza mkewe, ndiye aliyekimbiwa na mkewe kwa sababu ya kuzaliwa mtoto mwenye ulemavu.

Akiwa na mapenzi makubwa kwa  mwanawe huyo mwenye ulemavu wa viungo, humbeba kwa umbali wa kilomita kwenda na kurudi kutoka shule kila siku.

Iwapo kungekuwa na tuzo ya kumtafuta baba bora wa mwaka, bila shaka Yu angeibuka mshindi ijapokuwa wanaweza kuwapo kina baba wengine kumzidi yeye.

Juhudi na mapenzi yake hayo kwa mwanawe kuhakikisha hakosi elimu itakayomsaidia siku za usoni, ‘imelipa’ baada ya serikali ya eneo analoishi kuguswa na juhudi zake hizo.

Serikali imedhamiria kumsaidia baada ya vyombo vya habari vya jimbo la Sichuan kuandika habari zake.

Kila siku asubuhi Yu huamka saa 11 alfajiri akiandaa chakula cha mchana kwa ajili ya mwanawe awapo shule na kuondoka nyumbani saa 12 asubuhi, akimbeba mgongoni.

Hutumia saa zaidi ya mbili kutembea kuelekea shule na jioni saa 10 humchukua kutoka shule kurudi nyumbani kwa muda kama huo.

Kwa jumla, hutumia saa sita kila siku kwenda na kurudi kwa kuwa katika eneo la vijijini analoishi hakuna usafiri.

Yu Xukang anatembea umbali huo mrefu, huku mwanawe Xiao Qiang, akiwa mgongoni mwake katika kikapu maalumu alichotengeneza kwa ajili yake.

Baba huyo mwenye umri wa miaka 40 anaishi katika mji wa Fengyi katika kaunti ya Yibin, Jimbo la kusini magharibi mwa China la Sichuan, maili 2,000 magharibi mwa Shanghai.

Alikataa kusalimu kwa mvulana huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 12, pamoja na kwamba mikono yake miwili na miguu imepinda sawa na mgongo wake.

Alisema: “Najua mwanangu ni mwenye ulemavu wa mguu, lakini hana tatizo na ubongo wake. Hata hivyo, sikuweza kupata shule ya karibu yenye miundombinu ya kumkubali na kote nilikompeleka alikataliwa.

“Kwa kweli mahali pekee nilipoweza kupata ni Shule ya Msingi Fengxi katika mji huo wa Fengyi,” anasema.

Baba huyo alikimbiwa na mama wa mvulana huyo miaka tisa iliyopita wakati Xiao alipokuwa na umri wa miaka mitatu na akaamua kumlea peke yake.

Anasema amedhamiria kuona mvulana wake huyo haathiriki kwa kulelewa na mzazi mmoja na alitaka kumpatia fursa kwa kadiri ya uwezo wake.

Kwa sababu hakukuwa na basi la shule wala usafiri wa umma wa kufaa, baba huyo alionaa njia pekee ni kuhakikisha anambeba kila siku kwenda na kurudi shule.

Anasema: “Nambeba mwanangu kwenda shule na kurudi nyumbani tangu Septemba mwaka jana. Baada ya kufika shule natembea kuja hapa ili kufanya kibarua cha kunipatia chochote kisha natembea tena hadi shule kumchukua mwanangu na kurudi naye nyumbani.

Baba huyo anakadiria kutembea kilomita 2,500 akipanda na kushuka vilima tangu alipoanza kuhesabu.

“Mwanangu katika hali yake ya ulemavu hana uwezekano wa kutembea mwenyewe na hiyo inamaanisha hawezi kuendesha pikipiki.

“Pamoja na umri wake wa miaka 12, ana urefu wa sentimeta 90 tu. Lakini ninaona fahari kwa sababu tayari anashika nafasi ya juu darasani na atafanikiwa vitu vingi. Ndoto yangu ni kuona akienda chuo kikuu,” anasema.

Baada ya umbali ambao Xukang anatembea kufichuliwa  kwenye vyombo vya habari, serikali ya eneo hilo ilitangaza kuwa itakodi chumba kwa ajili ya baba huyo kuishi karibu na shule siku za usoni.

Pia shule hiyo itarekebishwa ili iweze kuchukua wanafunzi wa bweni, akiwamo Xiao, kusaidia kupunguza mzigo kwa baba.

Kwa mujibu wa Yu, madaktari wa kituo cha afya hadi hospitali ya jiji hawakuweza kubaini maradhi yaliyosababisha ulemavu wa mtoto huyo.

Kutokana na umbali wa kilomita 2,500 aliokwishatembea akipanda na kushuka mabonde, Yu ameshabadili pea tatu za viatu ndani ya nusu mwaka.

“Kamwe hatujawahi kuchelewa,” anasema kwa ufahari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles