Baada ya Urusi, Majaliwa atua Azerbaijan akiwakilisha JPM mkutano wa NAM

0
469

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa  anatarajiwa kumwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika Mkutano wa 18 wa Wakuu wa nchi na Serikali za nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) utakaofanyika Baku, Azerbaijan.

Awali, Majaliwa alikuwa Sochi nchini Urusi ambako pia alimwakilisha Rais Magufuli katika Mkutano wa Uchumi kati ya Urusi na Afrika (Russia – Africa Economic Forum) na baadae Mkutano wa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mataifa ya Afrika uliofunguliwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu  jana imeeleza kuwa mkutano wa NAM unalenga kujadili namna ya kutatua changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazokabili nchi wanachama katika nyakati za sasa.

Zaidi mkutano huo utajadili masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya nchi wanachama wa umoja huo.

Tayari Majaliwa amewasili nchini Azerbaijan tangu juzi na alipokewa na Naibu Waziri Mkuu wa Azerbaijan, Ali Ahmadov pamoja na viongozi wengeine wa Serikali hiyo katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heydar Aliyev.

Ajenda za mkutano huo ni kupokea ripoti za mkutano wa maandalizi wa Mawaziri, na ile ya maofisa waandamizi, uchaguzi wa nchi zitakazokuwa wajumbe katika ofisi ya uratibu wa shughuli za NAM, New York kwa kipindi cha mwaka 2019-2022. Majaliwa ameambatana na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika ya Mashariki, Dk. Damasi Ndumbaro na Balozi wa Tanzania Nchini Urusi ambale pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here