29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Baada ya kufunguliwa… Bila Chura, hakuna Snura Majanga  

snura6Na KYALAA SEHEYE

DUH! Siyo kwa kukomaa huko! Hivi ndivyo unavyoweza kusema mara baada ya kibao cha Chura, chake msanii Snura Mushi kuruhusiwa kuchezwa baada ya kuwa kifungoni kwa miezi kadhaa sasa.

Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ilifungia wimbo huo Mei, 4, mwaka huu kwa maelezo kwamba maudhui yake hayana maadili kwa jamii ya Kitanzania.

Katika maelezo ya Basata, Snura alitakiwa kutoshiriki kwenye shoo yoyote mpaka pale atakaporekebisha video ya wimbo huo na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake za muziki.

Lakini juzi, Jumatano Snura alisema kuwa wimbo wake huo umeshafunguliwa na serikali baada ya kurekodi upya video ya wimbo huo ambayo sasa ina maadili ya Kitanzania.

Kwa kawaida wasanii wengi ambao nyimbo zao hufungiwa, huachana nazo na kuendelea na nyingine, lakini kwa Snura imekuwa tofauti baada ya kuamua kukomaa hadi alipotimiza masharti yote na kuruhusiwa kuendelea na Chura wake.

Je, nini kimemfanya ang’ang’anie kwa nguvu zake zote kurejesha wimbo huo? Hiyo ndiyo sababu Swaggaz likaamua kuzungumza na Snura chemba ambaye hapa anafafanua:

“Nimekubaliana na maelekezo ya serikali na nimebadili video ya wimbo wangu wa Chura na sasa umeruhusiwa rasmi. Lakini najua watu wengi watakuwa wanajiuliza kwa nini nimeng’ang’ania huo wimbo? Kwanini nisingeendelea na nyingine nikaupotezea? Ukweli ni kwamba, Chura ndiyo kama utambulisho wangu.

“Bila Chura hakuna Snura, ndiyo maana nikaamua kutumia nguvu zangu zote kuurudisha. Kila mtu anafahamu kuwa Chura ndiyo wimbo wa kwanza wa Singeli kutamba kabla hata wanamuziki wengine hawajasikika.

“Wimbo huu uliniongezea mashabiki wa kila rika na Chura alikuwa gumzo kila kona hivyo kama mfanyabiashara sina budi kuweka mambo sawa ili nihakikishe naondoa hasara niliyopata wakati wimbo huo ulipofungiwa.

“Mashabiki bado wanaukubali sana na wanauhitaji, ndiyo maana nimeamua kutimiza yote urudi hewani. Angalia… wimbo ambao hausikiki kwenye redio wala runinga lakini upo midomoni mwa watu na huko mitaani bado unakiki kubwa.

“Halafu ukumbuke siyo hapa nchini pekee, hata nje ya mipaka ya nchi yetu. Juzi nimetoka Falme za Kiarabu, nilipotambulishwa nikatajwa kwa jina la  Snura Chura kwa hiyo naanza kuvuka mipaka ya nchi na Chura wangu.”

Swaggaz: Vipi kuhusu namna ya kucheza jukwaani ukiwa kwenye shoo. Itakuwa ya namna ileile au?

Snura: Uchezaji wangu utakuwa kama kawaida, stejini uno lipo palepale, ujue uno halikatazwi labda lile la kukiuka maadili na nisipocheza vizuri jukwaani huwa napigwa mawe, sasa hapo itakuwaje.

Mashabiki wajiandae kupokea shoo za maana, zenye mauno ya kufa mtu. Hatujakatazwa kukata mauno jukwaani maana hata ngoma zetu za asili zina viuno ila serkali imesisitiza maadili yatunzwe, jambo ambalo nitalifanya.

Swaggaz: Ulikuwa katika wakati gani baada ya wimbo wako kufungiwa? Hali ilikuwaje? Vipi kuhusu kibao chako kipya cha Shindu?

Chura: Niliumia sana Chura alipofungiwa kwani ndiyo wimbo wangu ulioanza kujulikana kimataifa, siyo siri nilishangaa sana kusikia hadi baadhi ya Wanigeria wanaujua na hilo ndiyo lilinisukuma zaidi kuhakikisha  wimbo huu unarudi tena hewani.

Kuhusu Shindu, umezungumzia maisha yetu sisi watoto wa Uswahilini, kwani hakuna msanii aliyewahi kuweka wazi maisha yetu… upo Kitanzania zaidi kwani Singeli ndiyo muziki wetu, Watanzania waupende na kuuheshimu, utatufanya tutoboe huo ndiyo ukweli.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles