27 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Baada ya BoT, mamlaka nyingine nazo zichukue hatua

HAKUNA shaka kwamba nchi yetu sasa inakabiliwa na changamoto kadhaa zilizotokana na maambukizi ya virusi vya corona na kutishia uchumi wake.

Tulisema huko nyuma kwamba pengine kutokana na umasikini, tunaamini zipo hatua nchi nyingi za kiafrika zingetamani  kuchukua ili kukabiliana na janga hilo kama ilivyo  kwa mataifa makubwa na yale ya kati duniani.

Tulisisitiza kwamba hatua za kukabili hali ngumu ya uchumi zinahitajika mapema na wiki hii Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanya uamuzi mkubwa.

BoT imetangaza kuchukua hatua sita za kisera kukabiliana na athari za corona kwenye benki ikiwa ni pamoja na kupunguza riba, amana, hati fungani na dhamana.

Kwa mujibu wa taarifa ya benki hiyo, uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya BoT na kutoa ahueni kwa taasisi za fedha.

Ilibainisha kuwa lengo la hatua hizo ni kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha na upatikanaji wa huduma za fedha nchini.

Hatua zilizochukuliwa ni kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa BoT kutoka asilimia saba hadi sita, kuanzia Juni 8.

Wakati BoT wakichukua hatua hiyo, tuliandika huko nyuma kwamba tayari baadhi ya watu biashara au kazi zao zimeathirika kutokana na ama kufunga au kushuka hasa kwa wakati huu.

Upo ushahidi mwingi wa biashara kuporomoka  kutoka kwa wenye vituo vya mafuta, wauza nguo, wakulima wakubwa ambao  wengine mazao yao waliyokuwa wakisafirisha nje ya nchi sasa yanaoza kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka.

Miongoni mwa hao  tulisema wapo ambao walichukua mikopo mikubwa katika taasisi za fedha na sasa hali imekuwa tofauti.

Watu hao hao na wengine ndio wanaokabiliwa na madeni makubwa ya pango na mengine.

Tuliona Serikali ya Kenya ikitangaza kuchukua hatua ili kuwanusuru raia wake ambao wameyumba kiuchumi katika wakati huu.

Miongoni mwa hatua ambazo Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilichukua ni pamoja na kutenga fedha kwa kaya zisizojiweza.

Lakini pia imetangaza Mamlaka ya Usambazaji wa Tiba kuondoa masharti ya ununuzi wa vifaa vya kujilinda dhidi ya Covid-19  kwa takriban miezi mitatu ili kurahisishia raia kununua vifaa hivyo.

Wakati Kenya ikichukua hatua hizo huko nyuma tumeona Marekani ikiongeza tena dola nusu bilioni mbali na zile dola trilioni mbili kwa raia wake waliopoteza ajira katika wakati huu wa janga la corona.

Hatuwezi kamwe kujilinganisha na Marekani kwa uwezo na kila kitu, lakini tunachotaka kusema pamoja na hatua zilizochukuliwa na BoT, mamlaka nyingine za Serikali nazo zifikirie namna ya kuwapunguzia mzigo wananchi wake kama ambavyo tumeona Kenya, hususani kwenye suala zima la kodi.

Tunasema hivyo kwa sababu tunaamini bila kufanya hivyo, wengi wataumia na watalazimika kufunga biashara na huko mbele Serikali ikajikuta imepoteza walipakodi wengi zaidi.

Hali kadhalika ianze kufikiria jinsi ya kusaidia watu wasiojiweza ambao tuna hakika katika wakati huu maisha yamezidi kuwa magumu kwao, hasa kwa kuzingatia kwamba lipo kundi kubwa la Watanzania ambao kujiwekea akiba kwao ni mtihani kutokana na hali ngumu ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo kila wakati.

Ndiyo maana tunasema Serikali ianze kufikiria namna ya  kunusuru mambo kama hayo kwa wakati huu kabla mambo hayajawa mabaya kabisa kwa sababu hakuna anayeijua kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,454FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles