24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Azikwa baada ya kukaa mochwari miezi minane

Na ELIUD NGONDO- MBEYA

FAMILIA ya kijana Frank Kapange (22) imeuchukua mwili wa mtoto wao katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, baada ya kukaa miezi minane na siku 22 katika chumba cha kuhifadhia maiti kutokana na kuibuka sintofahamu ya kifo chake.

Akizungumza hosptalini hapo, msemaji wa familia, Julius Kapange, alisema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya mahakama kuamuru familia kuzika mwili huo ndani ya wiki moja vinginevyo jiji lifanye shughuli hiyo.

Alisema kutokana na uamuzi huo wa mahakama, wameamua kumzika kijana wao japo wanaamini haki haijatendeka kwani alipatwa na mauti akiwa katika kituo cha polisi.

 “Leo tumechukua mwili wa kijana wetu, tunaenda kuzika kijijini kwetu Syukula Rungwe. Sababu ya kufanya hivyo ni kwamba mahakama ilitutaka tuzike kabla ya wiki moja, hivyo tukaona ni vyema tufanye hivyo kuliko kuendelea kumtesa mwanetu, lakini mpaka tumefika hatua hii mahakama haijatutendea haki katika kuamua kesi yetu,” alisema Kapange.

Kapange alieleza kuwa kijana wao katika historia ya maisha yake hakuwahi kuwa na matukio ya uovu, hivyo wamepata pigo kwenye familia kwani yeye toka alivyokuwa amehitimu kitado cha nne, alikuwa ni msaada mkubwa kwao.

Ameongeza kuwa siku ya Jumapili waliitwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Godlove Mbwanji, na waliambiwa wakauchukue mwili wa kijana wao na gharama za kuhifadhia maiti hiyo kwa muda wote wamesamehewa.

“Sisi tulienda mahakamani kuomba mwili wa mtoto wetu uchunguzwe kwani kifo chake kilikuwa ni cha utata na siyo kususia kama wengine wanavyosema, baada ya mazishi tutaendelea kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo,” alisema Kapange.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mbwanji alisema wameamua kusamehe gharama za kutunzia maiti hiyo kwa muda wote ili fedha ambazo waliziandaa zikatumike kwenye msiba.

Alisema gharama za kuhifadhi mwili hospitalini hapo kwa siku ni Sh 20,000, hivyo kwa siku ambazo ulikaa, ungetakiwa kulipiwa zaidi ya Sh milioni 5.2.

Mama wa marehemu, Monica Kapange, alisema mwanawe alikuwa akimsaidia katika kuuza duka lake, lakini siku anapatwa na tukio hilo, alikuwa ametoka msibani kumzika rafiki yake ndipo alipokamatwa na polisi wakaondoka naye.

Alisema baada ya kupewa taarifa kuwa mwanawe amekamatwa, aliwasiliana na kijana wake wa kwanza ambaye alienda Kituo Kidogo cha Polisi Mwanjelwa na kuambiwa Frank amepelekwa Kituo kikubwa cha Polisi.

Monica alisema baada ya kijana wake wa kwanza kwenda katika kituo hicho, jioni aliambiwa Frank amefariki dunia hali ambayo ilianza kuleta utata wa kifo hicho.

 “Kijana wangu wa kwanza alienda kituo cha polisi mjini kwenda kumtazama kaka yake, lakini jioni aliambiwa kaka yake amefariki hali ambayo ilitia simanzi kubwa ndani ya familia,” alieleza mama huyo.

Shangazi wa marehemu, Sophia Kapange, alisema alikuwa akifuatilia kesi ya kijana huyo akisubiri haki itendeke juu ya kifo hicho, lakini walikuwa wakipigwa danadana hadi kuamuliwa wakauzike mwili huo.

Sophia alisema mahakama haijatenda haki juu ya kijana huyo aliyeuawa akiwa mikononi mwa polisi na badala yake imetoa uamuzi wa kibabe.

Alisema wameamua kuuzika mwili huo baada ya kuambiwa wasipouzika manispaa itauzika na wao wakaona kuwa kijana wao asingeweza kuzikwa na manispaa kwani hakuwa na makosa yoyote katika jamii.

Frank alifariki Juni 4, mwaka jana huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido jijini Mbeya alifariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi, hivyo waligoma kumchukua kwenda kumzika.

Kutokana na ndugu hao kuona ukakasi wa kifo cha kijana wao, walitaka kujiridhisha pasipo shaka juu ya kilichosababisha, hivyo wakafungua shauri Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya itoe amri ya kufanyika kwa uchunguzi rasmi wa kisheria wa kifo cha kijana wao.

Lakini mahakama hiyo Agosti mwaka jana ilitupilia mbali shauri hilo baada ya kuona shauri hilo limekosa mashiko na kuamuru mwili huo kuzikwa na ndugu wanahitajika kubeba gharama zote za mazishi.

Ndugu walidai kutoridhika na uamuzi huo, wakaamua kukataa rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo Novemba mwaka jana ilitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kuifungua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,093FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles