Azam yatamba kuiua Yanga Ngao ya Jamii

JO6A0307

Na DOREEN PANGANI (TUDARCO) – DAR ES SALAAM

ZIKIWA zimebaki siku mbili kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Azam FC dhidi ya Yanga, uongozi wa miamba hiyo ya Chamazi umeweka wazi dhamira yao ya kunyakuwa taji hilo ambalo huashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam, Jafari Iddy, alisema wamepania kushinda pambano hilo ili kurudisha heshima na mafanikio katika klabu hiyo.

“Ni mchezo ambao utawapa nafasi wachezaji wapya kuonekana na kujulikana kwa kikosi cha kwanza cha Azam FC kilichosukwa upya na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez.

“Hatuna presha juu ya ushindi katika mchezo huo kwani tuna uhakika wa kurejesha heshima kabla ya kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Iddy.

Kwa upande wake kocha mpya wa Azam, Hernandez, alisema ana uhakika wa kuifunga Yanga kwenye mchezo huo.

“Siwezi kuzungumzia sana mechi ya Yanga,” alisema Hernandez na kuongeza:

“Ninaamini jitihada zangu na taaluma ninayowapa wachezaji wangu itazaa matunda.

“Lakini natambua ya kuwa Yanga ni kongwe na inacheza vizuri, kikubwa naamini nitashinda mchezo huo kulingana na kile ninachowapa wachezaji wangu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here