Na WINFRIDA NGONYANI – DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Azam FC umetoa baraka zote kwa mshambuliaji wake, Kipre Tchetche, aliyejiunga rasmi na klabu ya Al-Nahda Al-Buraimi ya nchini Oman.
Hivi karibuni Kaimu Mwenyekiti wa Azam FC, Idrissa Nassor, alinukuliwa akisema kuwa wapo tayari kumuuza mshambuliaji huyo kwa dau la Dola za Kimarekani 150,000 (sawa na Sh milioni 322) na kwamba hakuna klabu ya Tanzania inayoweza kutoa fedha hizo.
Mshambuliaji huyo aligoma kurejea Azam FC na kutimkia kwao Ivory Coast wakati akiwa na mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo iliyokuwa ikimhitaji kukitumikia kikosi hicho.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffer Idd, alikanusha uvumi uliosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa mshambuliaji huyo amejiunga kimya kimya na klabu hiyo.
“Kipre ameondoka kwa makubaliano maalumu na si kama watu wanavyodai, sisi tumemalizana nao kwa kufuata sheria zote,” alisema Idd, ingawa hakutaja mkataba wa miaka mingapi.
Picha za mshambuliaji huyo ambaye alijunga na Azam mwaka 2011, zimemuonyesha akikabidhiwa jezi namba 10 ambayo alikuwa akiitumia tangu akiwa Azam.
Wakati huo huo, Azam FC Jumamosi itacheza mchezo wa kirafiki na timu ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani.