23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Azam macho kileleni, Simba heshima

simba-sports-club-212HERM5672-1NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo ambapo timu ya Azam itajitupa uwanjani kuvaana na Mgambo Shooting Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kusaka nafasi ya kurudi kileleni mwa ligi, wakati Simba wakitarajia kupepetana na maafande wa JKT Ruvu Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Azam FC inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 sawa na Yanga inayoongoza kwa pointi hizo, lakini ikitofautiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. Simba yenyewe inashika nafasi ya tatu ikiwa imejikusanyia pointi 30.

Mchezo wa Azam FC na Mgambo unatarajiwa kuwa wa kukata na shoka, kwani maafande hao hawapendi kuruhusu kufungwa katika uwanja wao wa nyumbani na pia itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuitandika JKT Ruvu bao 5-1, lakini pia wana lambalamba hao katika mchezo uliopita walilazimishwa sare ya bao 1-1 na African Sports katika Uwanja wa Chamazi Complex hivyo kufikisha sare tatu.

Kocha wa Azam, Stewart Hall, juzi alitumia dakika 30 kukisoma kikosi cha maafande hao walipokuwa wakifanya mazoezi chini ya kocha wao Bakari Shime, ili kuangalia wapi pa kuwadhibiti katika mchezo wa leo.

“Mgambo si timu rahisi, tutacheza nao kwa tahadhari, ni mchezo mgumu lakini nia yetu ni kushinda ili kuweza kuwa juu katika msimamo wa ligi, huu si wakati wakudondosha pointi hata moja,” alisema.

Azam itawakosa wachezaji wao mahiri akiwemo Allan Wanga, Didier Kavumbagu, Ramadhani Singano ‘Messi’ ambao ni majeruhi, wakati Hamis Mcha ana matatizo ya kifamilia.

Simba wao watashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 walioupata kwa Mtibwa. Mchezo huu utakuwa wa pili kwa kocha Jackson Mayanja aliyeichukua timu hiyo wiki iliyopita mikononi mwa Mwingereza, Dylan Kerr.

Mayanja ameeleza iwapo viongozi wa klabu hiyo watawatimizia wachezaji mahitaji yao ya msingi, ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu lazima utatua Msimbazi.

Kocha huyo aliliambia MTANZANIA jana kuwa viongozi wanatakiwa kufahamu wachezaji wanahitaji nini ili kuwajengea mazingira ya kutekeleza ipasavyo majukumu yao uwanjani na nje ya uwanja.

“Wachezaji watakapopata sapoti kutoka kwa viongozi pamoja na mashabiki, itawasaidia wao kuongeza morali ya kufanya vizuri na kuifanikisha timu kuchukua ubingwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mayanja amesema kuwa beki wake wa kulia, Hassan Kessy, anatarajiwa kurejea uwanjani leo, lakini Simba huenda ikamkosa mshambuliaji, Ibrahim Ajib ambaye aliumia katika mchezo wao na Mtibwa.

JKT Ruvu inayoongozwa na kocha Abdalah Kibadeni, itaingia uwanjani ikiwa na mawenge kufuatia kichapo cha bao 5-1 dhidi ya Mgambo JKT. Maafande hao wapo katika nafasi ya 11 ikiwa pointi 14 kwenye msimamo wa ligi.

Mechi nyingine kesho itakuwa kati ya Stand United na Toto Africans Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, wakati Prisons ikiiwinda Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles