NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Azam FC, leo wanatarajia kufunga ratiba zao za mechi za kirafiki kwa kujipima tena na wanajeshi timu ya Ruvu Shooting, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Hivi karibuni Azam ilipokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu na kuvurugiwa rekodi ya kutokufungwa bao hata moja ndani ya dakika 90 katika michuani ya Kagame.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jaffari Idd, alisema mchezo huo utahitimisha ratiba zao za mechi za kirafiki na kuendelea na programu nyingine za mazoezi, wakijiandaa kufungua pazia la ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons Septemba 12, Uwanja wa Chamazi.
“Tutacheza na Ruvu Shooting ukiwa ndio mchezo wetu wa mwisho wa mechi zetu za kirafiki, tutampa nafasi kocha kurekebisha mapungufu kiasi yaliyojitokeza ili tuingie kamili kwenye ligi,” alisema.
Alisema, kwa ujumla kikosi chao kipo imara, kwani wachezaji wana morali tangu watwae ubingwa wa Kagame kwa mara ya kwanza, wanaonyesha kiu ya kuutaka ubingwa wa ligi kuu, nina imani ndivyo itakavyokuwa.