Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
MICHUANO ya Kombe la Shirikisho inatarajiwa kuendelea leo kwa timu ya Azam kuvaana na KMC ya Kinondoni katika Uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam, Singida United wakiwakaribisha Polisi Tanzania kwenye dimba la Namfua, Singida.
Azam FC waliingia kwenye hatua ya 16 Bora baada ya kuifunga Shupavu FC mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, huku KMC wakiwafunga Toto Africans mabao 7-0 katika dimba la Uhuru Dar es Salaam.
Singida United waliwafunga Green Warriors, kwa jumla ya mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia kutoka suluhu ndani ya dakika 90, wakati Polisi Tanzania waliiondoa Friends Rangers baada ya kuifunga mabao 2-1.
Azam FC watakuwa na hasira ya kuhitaji ushindi kutokana na kuvurunda katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hiyo itaendelea kumkosa nahodha wao, Himid Mao, ambaye ni majeruhi anayesumbuliwa na goti pamoja Waziri Junior.
KMC timu ambayo imefanikiwa kupanda ligi kuu msimu ujao, imepania kuweka rekodi nzuri msimu huu, hivyo hawatakubali kufungwa kirahisi na kuiaga michuano hiyo.
Upande wao Singida United timu ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu, watashuka dimbani wakihitaji ushindi baada ya mchezo wao wa mwisho wa ligi kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye dimba la Kaitaba mkoani Kagera.
Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Azam FC, Iddy Cheche, alisema malengo yao ni kushinda ili kufanikiwa kuvuka kwenye hatua inayofuata.
Upande wake Kocha wa KMC, Fredy Minziro, alisema watapambana hadi mwisho kuhakikisha wanawakalisha chini Azam FC.
“Azam ni timu kubwa hivyo ukifanya mchezo unaweza ukapoteza mchezo na sisi tumejipanga kuhakikisha tunawakabili ili tupate matokeo yatakayotuvusha kwenye hatua hii,” alisema.
Kocha wa Singida United, Hans van der Pluijm, alisema licha ya ratiba kubana haitawafanya washindwe kupata matokeo mazuri, kwani wamejipanga kufanya vizuri na kupata ushindi mnono.