AZAM FC YAITESA YANGA

0
630
Waziri Junior akikabidhiwa jezi namba 7 na meneja wa timu ya Azam FC, Philip Alando

 

 

Na MARTIN MAZUGWA-DAR ES SALAAM

MABINGWA wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, timu ya Azam FC, imeipiga kumbo Yanga baada ya kumsajili kiungo mkabaji wa Mbao FC, Salmin Hoza kwa miaka miwili.

Hilo ni pigo jingine kwa Yanga, baada ya juzi Azam FC kumsainisha mshambuliaji Mbaraka Yusuph kutoka Kagera Sugar, ambapo awali walimsainisha Waziri Junior kutoka Toto Africans ya Mwanza.

Yanga imekuwa katika mipango ya kuwasajili wachezaji hao, Hoza, Yusuph na Junior, ambao sasa wataonekana wakiitumikia Azam FC msimu ujao, yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Itakumbukwa kuwa Waziri Junior aliwahi kwenda makao makuu ya klabu ya Yanga, Mtaa wa Twiga na Jangwani na kupiga picha akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, Salum Mkemi na kushikishwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini siku iliyofuata akaenda kusaini Azam FC na kuwaacha solemba mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Hoza alikuwa katika mipango ya kutua Yanga, ambapo alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, lakini walishindwa kuafikiana.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili baada ya kusaini mkataba huo, Hoza alisema ameamua kujiunga na Azam FC ili aweze kupata nafasi zaidi ya kucheza na kuendeleza kipaji chake, lakini pia ikiwa njia ya kwenda kucheza soka nje ya nchi.

“Kila mchezaji anayechipukia huwa na ndoto za kucheza timu kubwa ili kupata nafasi ya kuonekana na timu za nje ya nchi, nafurahi kujiunga hapa, naamini nitafika mbali,” alisema Hoza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here