25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Azam FC yaiongezea maumivu KMC

  • Yanga Ruvu shooting watatafutana leo

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

WAKATI Yanga ikitarajia kushuka dimbani leo kuivaa Ruvu Shooting, Azam FC imezindua kwa kicheko kampeni zake za msimu mpya, baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Uhuru , Dar es Salaam.

Bao pekee lililoipa pointi tatu Azam, lilifungwa na mshambualiaji wao hatari, Iddy Seleman ‘Nado’ dakika ya 14, baada ya kumalizia krosi safi ya Nicolas Wadada.

Ushindi wa Azam umeiongezea machungu KMC, ambayo hivi karibuni ilitupwa nje ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuchapwa jumla ya mabao 2-0 na AS Kigali ya Rwanda, ikianza kulazimisha suluhu ugenin, kisha kupigwa mabao 2-0 Uwanja wa Taifa.

Kwa upande wake, Yanga itaivaa Ruvu Shooting leo ikiwa na mzuka wa kutosha unaotokana na kufuzu hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuiondoa mashindanoni timu ya Township Rollers ya Botswana, kwa ushindi wa mabao 2-1, ikianza kulazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kushinda bao 1-0, jijini Gaborone.

Kwa kuzingatia hilo, vijana hao wenye maskani yao Jangwani jijini Dar es Salaam, watataka kupata ushindi katika mchezo huo, ili kuendelea kuwapa raha mashabiki wao sambamba na kufufua matumaini ya kurudisha taji la Ligi Kuu kwenye milki yao, baada ya kulikosa kwa misimu miwili mfululizo.

Yanga inajivunia rekodi nzuri inapokutana na Shooting, kama ambavyo ilikutokea msimu uliopita iliposhinda michezo yote miwili hivyo kuvuna pointi sita.

Ilianza kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Shooting katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Disemba 12, mwaka jana, Uwanja wa Taifa kabla ya kuwazamisha tena wanajeshi hao kwa kuwapa kichapo cha bao 1-0, walipokutana nayo mzunguko wa pili, mchezo uliochezwa Mei 12, mwaka huu, Uwanja wa Uhuru.

Shooting inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), itauanza msimu huu ikiwa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Salumu Mayanga, ambaye alirithi mikoba ya Abdulmutik Haji.

Mayanga atataka kuwaonyesha mabosi wake kwamba hawakukosea kumpa jukumu hilo, kwa kuingiza timu uwanjani huku akiwa na dhamira ya kufuta uteja kwa Yanga.

Yanga itakosa huduma ya mabeki wawili, Paulo Godfrey anayeuguza jeraha la paja na Mwarami Issa aliyemia kabla ya mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha wa Yanga , Mwinyi Zahera alisema mipango yake ni kuhakikisha anapata ushindi ili kuunza vema msimu mpya wa ligi hiyo.

“Hii ni mechi ya kwanza ya ligi, ni muhimu kushinda ili kufungua vema hesabu zako, tumetoka kupata ushindi ugenini kitu ambacho kinatupa nguvu na morali ya juu.


“Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, hatukuweza kupumzika tuliingia kambini mara moja, tumepanga kupata pointi tatu ili kujiweka vizuri katika mbio za kuwania ubingwa.

Msimu huu ushindani utakuwa mkali, hivyo mikakati inatakiwa kuanza mapema,” alisema kocha huyo mwenye Uraia wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) na Ufaransa.

Kwa Upande wake, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema wamejizatit kuhakikisha wanapata ushindi na kuvuna pointi tatu dhidi ya Yanga.

“Wachezaji wamekaa kambini kipindi kirefu wakifanya mazoezi ili kujiweka katika hali ya ushindani, tuna mwalimu mzuri ambaye anajua namna ya kupata matokeo kwenye mechi kama hizi, hatuna shaka hata kidogo.

“Tunajua ukubwa na ubora wa Yanga, lakini safari hii tunakuja kivingine, hawawezi kutusumbua, nina hakika tutafungua vema msimu,”alisema Bwire.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles