AZAM FC SASA SOKA LIMEWASHINDA, BAKINI KWENYE VIWANDA

0
651

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM


WIKI iliyopita suala kubwa lililoonekana kuchukua nafasi kwenye mitandao ya kijamii ni juu ya uongozi wa timu ya Azam kuachana na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wao, Saad Kawemba, pamoja na nahodha wa timu hiyo, John Bocco.

Siku chache baadae, Azam, kupitia kwa msemaji wao ilitangaza kutowaongezea mikataba wachezaji Ame Ally, pamoja na Khamis Mcha, ambaye ni mmoja wa wachezaji wakongwe ndani ya timu hiyo.

Achana na hilo. Pia kuna linalotajwa, kuwa ni suala la mgogoro wa chini kwa chini unaosababishwa na baadhi ya viongozi. Mgogoro unaoonekana kuwaathiri na wachezaji wao, ambao sasa wameonekana kutohitaji kuongeza mikataba mipya.

Kutokana na mwenendo wa Azam hivi sasa ,kila mdau wa soka anaonekana kuzungumza yake, lakini walio wengi wanawaza wapi inapoelekea timu hiyo.

Kwa mtazamo wa haraka haraka unaweza kusema ni sawa ama si sawa kwa uongozi kuachana na baadhi ya watu wake walioiletea mafanikio, lakini pia kuamua kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa hawapo kwenye mashindano ya kimataifa, ila suala la kujiuliza ni wapi  timu hiyo inaelekea?

Inaeleweka wazi Azam  FC ni moja ya timu zilizoleta changamoto kwa wakongwe wa soka  hapa nchini, Simba na Yanga.

Kiroho safi inaamini  mwenendo wa timu hiyo umeanza kuonekana  msimu uliopita, walioamliza katika nafasi ya nne nyuma ya timu za Kagera Sugar, Yanga na Simba, hivyo kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ni wazi tayari Azam kuna tatizo.

Ni ukweli usiofichika soka ni biashara, hivyo suala la kupunguza gharama halizuiliki. Kitendo cha Azam kutaka kupunguza bajeti yao ya uendeshaji ni dalili za kushindwa kuiendesha timu katika mipango ya kusonga mbele, kama walivyojipanga awali.

Huenda ni kweli Azam imeyumba kiuchumi, kulingana na hali halisi iliyopo hivi sasa kwa Watanzania wengi, lakini sidhani kama ni sababu kubwa ya kuondoka kwa wachezaji muhimu kama Bocco, Manula anayetajwa kutaka kujiunga na Simba, Himid Mao, Shomari Kapombe na wengineo ambao mikataba yao inafika ukingoni.

Zipo taarifa zinazosema kuwa wanandinga hao wanaondoka na wengine,  huku wengine wakiondoka baada ya kushindwa kueleweana na uongozi katika suala la mikataba mipya.

Sawa, Azam wameshindwa kumbakisha Bocco kwenye timu yao, hadi kwa Manula, Mao, Mcha? wachezaji  ambao wametoka mbali na timu hiyo. Wamevuka milima na mabonde hadi leo hii kuwa miongoni mwa timu zinazojulikana Barani Afrika.

Kama ni hivyo, dalili zimeshaonekana wazi uongozi wa Azam unakoelekea ni kushindwa kuiendesha timu.

Ni bora wakaamua kubaki katika uendeshaji wa viwanda vyao vya kuzalisha Maziwa, Unga, Ice Cream, Maji, Nazi, Chapati na Juisi pekee, ili soka libaki kwa wale waliozoea figisu figisu na mchakamchaka wa kuliendesha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here