30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

AWESO:  SH 10,000 YA MAMA ILITIMIZA NDOTO YA KUWA MBUNGE 

*Asema alitamani ubunge baada ya mpita njia kujifungua mlangoni kwao

Na ELIZABETH HOMBO-DODOMA


JUMA Aweso ni miongoni mwa wabunge vijana walioingia katika Bunge la 11 ambaye alimwangusha Mbunge wa siku nyingi wa Jimbo la Pangani, Salehe Pamba katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Baadaye alipambana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na kufanikiwa kumshinda.

Jumatatu wiki hii MTANZANIA lilifanya mahojiano na Aweso ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia changamoto alizokumbana nazo katika uchaguzi huo.

MTANZANIA: Hebu tueleze historia yako kwa ufupi kwa faida ya Watanzania wasiokufahamu.
AWESO: Naitwa Juma Aweso ni mtoto wa pili kati ya watoto sita. Nimehitimu Shahada ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2013. Shule ya Sekondari nimesoma Pugu na kidato cha tano na sita nimesema Shule ya Sekondari Bagamoyo. 

MTANZANIA: Ni kitu gani kilichokushawishi kuingia kwenye siasa?

AWESO: Nakumbuka nikiwa mdogo wakati huo nilikuwa darasa la pili, siku hiyo ilikuwa saa nane usiku tumelala akaja mama mmoja ambaye ni mjamzito alikuwa na watu watatu wa familia yake.

Sasa walikuwa wanataka kuvuka kivuko lakini muda ule ilikuwa kimefungwa, unajua nyumba yetu iko karibu na kivuko.

Yule mama na familia yake baada ya kuona kuwa kivuko kimefungwa wakaja nyumbani kwetu  wakagonga mlango huku wanalia, sasa ile mama anatoka tu yule mama akajifungua pale pale mlangoni.  

Kwa bahati mbaya yule mama akafariki dunia lakini mtoto wake alikuwa mzima niliumia sana japo nilikuwa mdogo, mama alikuwa ananifukuza niingie ndani lakini mimi nilikuwa nafuatilia kila kitu nikiwa ndani huku nalia.

Mama yangu ni mama lishe, sasa asubuhi wakati nipo pale hotelini kwa mama kwa sababu huwa namsaidia kazi mbalimbali, nikamwambia nitasoma mpaka nifikie chuo kikuu ili niwe mbunge nije nisaidie jamii yetu ili wengine wasikutwe na haya yaliyomkuta yule mama aliyejifungua mlangoni akafa.

Kingine kilichonifanya nijitume zaidi ni kwa sababu baba yangu na mama walitengana na bahati mbaya baba alifariki dunia mwaka 2010, kwa hiyo sisi tulikuwa na mama na yeye ndiye aliyetuhangaikia na kutusomesha.

Wakati wanatengana mimi na dada yangu tuliyefuatana wote tulikuwa sekondari hivyo ilifikia hatua mama ikabidi auze kitanda na cheni zake ili atulipie ada.

Sasa namna nilivyoingia kwenye siasa; nikiwa pale UDSM niliteuliwa kuwa mwenyekiti wa wakemia kwa maana ya kuwatetea na nilifanya kwa uadilifu mkubwa sana ikafika wakati wale wanaomaliza masomo hayo wengine wanachukuliwa na kupangiwa kazi pale pale chuoni.
Sasa baadaye mwaka 2012 nikawa nimeenda likizo nyumbani nikakuta ni wakati wa uchaguzi wa ndani wa NEC Pangani. Nikaenda kwenye kopo la mama anakoweka fedha nikachukua Sh 10,000 kwa ajili ya fomu kugombea nafasi ya mjumbe wa NEC, lakini wakaniambia mimi mdogo sana sitaweza nafasi hiyo lakini nilikomaa mpaka jina langu likapita.

MTANZANIA: Sasa ulivyochukua Sh 10,000 ya mama, ulimwambia?

AWESO: (Anacheka) kwa kweli sikumwambia lakini baadaye akaulizia sana kuwa nani amechukua Sh 10,000 kwenye kopo lake mimi nikamwambia sifahamu.

Nilikuwa na malengo makubwa kutokana na changamoto zilizopo pale Pangani na nilikuwa na moyo kabisa wa kuisaidia jamii yangu ya Pangani. Sasa majina yakaenda kwenye Kamati Kuu na jina langu likapita kati ya majina matatu.

Katika majina hayo matatu, alikuwapo Mwenyekiti wa CCM Pangani na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi lakini kwa bahati mimi nikashinda.

Baada ya kushinda kukawa na vikao vya NEC kwa siku tukawa tunapewa Sh 80,000 nikamnunulia mama simu nikampa na Sh 50,000. 

Sasa siku hiyo ndiyo nikamwambia mama ukweli kuwa Sh 10,000 yake iliyopotea nilichukua ili nigombee nafasi ya mjumbe wa NEC akabaki anacheka tu. 

Baada ya kumaliza chuo mwaka 2013 nikarudi pale nyumbani nikajitolea kufundisha shule za kata. Wakati huo mama akawa analalamika kuwa pamoja na kunisomesha mbona haoni matunda hata kupata kazi.  Nikamwambia nataka nigombee ubunge akasema hutaweza mwanangu kwa sababu ubunge unahitaji fedha.

Sikukata tamaa. Nikachukua fomu na wagombea tulikuwa 11 kwenye kura za maoni lakini kuna watu wakawa wananidharau kuwa mimi ni mdogo hivyo sitaweza. Nikawa nawaambia kuwa sindano ndogo lakini ndiyo inashona madera na makoti.

MTANZANIA: Ni changamoto gani ulizokumban anazo katika uchaguzi huo?

AWESO: Kwa kweli ushindani ulikuwa mkubwa, fitna, nilikuwa sina fedha kabisa hata karatasi za kubandika nilikuwa sina lakini watu wenye nia njema na familia wakanisaidia. Nikashinda kwa kishindo.

Changamoto kubwa nyingine kuna wapambe wa wagombea wengine (wakati wa kura za maoni) walikuwa wanamfuata mama yangu kuwa anishawishi kuwa nisigombee ikafikia hatua wakawa wanampelekea mchele, ngano kutokana na shughuli zake anazozifanya.

Baada ya mama kushindwa kunishawishi wakanitumia ujumbe wa maneno kuwa kama bado mbishi nitaparapooaz mwili au nitakufa kabisa. Huo ujumbe wakawa wanamtumia mama pia. 

Kwa kweli hali aliyokuwa nayo mama wakati ule siwezi kuelezea maana kila siku alikuwa analia na kuniomba niache. Lakini sikukubali.

MTANZANIA: Sasa baada ya kutumiwa ujumbe wa vitisho ulichukua hatua gani?

AWESO: Sikuchukua hatua zozote zaidi ya kujiamini na kumwomba Mungu.
Baadaye nikapambana na aliyekuwa Mwenyekiti wa PAC, Amina Mwidau akigombea kwa tiketi ya CUF naye nikamshinda.

MTANZANIA: Pamoja na hayo ni jambo gani ambalo lilikuumiza zaidi katika uchaguzi huo?

AWESO: Usaliti ndani chama changu kwa sababu baada ya kuwashinda wale wagombea ndani ya chama badala ya kuniunga mkono lakini hawakuwa pamoja na mimi, walinitenga. 

Kwa sababu utaratibu wa kawaida anavyopatikana mgombea ndani ya chama lazima wengine wamuunge mkono lakini kwangu haikuwa hivyo. Hiyo iliniumiza.

MTANZANIA: Na ulivyoshinda ubunge mama alipokeaje?

AWESO: Mama alilia sasa akawa haamini na hadi leo haamini kilichotokea.

MTANZANIA: Wakati unagombea ubunge ulitoa ahadi gani kwa wananchi wako wa Pangani ambayo umeyatekeleza?
AWESO: Kuna vitu vilikuwa vinaniumiza; kwanza suala la elimu pale Handeni kulikuwa hakuna hata kidato cha tano kwa mchepuo kwa masomo ya sayansi.

Kupitia kauli mbiu ya ‘Niache Nisome’ tukawa tunahamasisha elimu. Kama mbunge katika kuhamasisha elimu nimetoa mifuko ya saruji 1,500.

Unajua mwaka 2005 Wilaya yetu ya Pangani ilipata cheti cha mwisho kielimu kimkoa lakini sasa tunashukuru kutoka nafasi 12 kati ya 12 sasa tumefikia nafasi ya tano kati ya 12.

Pia tulikuwa tuna shule za sekondari mbili za serikali lakini hivi sasa tunazo saba huku binafsi zikiwa mbili.
Changamoto nyingine ni afya ambapo watu wa Pangani wanafuata vipimo vya X’ray Tanga Mjini lakini sasa Waziri wa afya, Ummy Mwalimu alitutembelea pale ametuahidi tutapata kipimo hicho hivi karibuni.

Pia kwa upande wa umeme kuna baadhi ya maeneo yalikuwa hayana umeme tayari tumeweka umeme katika maeneo hayo na sasa bado vijiji vichache.
Changamoto nyingine kubwa ni barabara ambapo Waziri Ummy pia amefika na ameahidi katika bajeti hii wataliingiza.

Kingine ni kivuko cha Mv Pangani kilikuwa kibovu lakini baada ya kupambana tumepata kipya kinaitwa Mv Tanga na tukapewa na boti. 

Kwa upande wa maji, Mto Pangani unatiririsha maji tukasema uwekwe mradi mkubwa wa maji lakini bahati nzuri Taasisi ya dini ya Islamic Help wameandika mradi na tumepata gari letu wenyewe kuchimbia visima.

Kwa hiyo sasa tutachimba visima maeneo ambayo hayana maji. Wakati sisi tunaendelea kuibana serikali nikafanya jitihada ya kupata gari kupunguza uhaba wa maji. 

Pia Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alitupa milioni 200 kwa ajili ya maji. Kwa upande wa kilimo, tulikuwa tunategemea zao la mnazi na nitauliza swali bungeni kuwa serikali ina mkakati gani kuhusu zao la mnazi kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi hivyo tuweke zao mbadala ya korosho ili kuinua uchumi wa Pangani.
Pia Islamic Help wametupatia treka kwa ajili ya kuwasaidia wakulima hasa wale wenye hali duni.
Changamoto nyingine bado watu ni masikini hivyo uwezeshaji wa halmashauri na zile Sh milioni 50 kwa kila kata serikali itoe kwa wakati.
Kingine ni kuhusu bahari tunahitaji uwezeshaji wa wavuvi kwa sababu tunaona serikali inawasaidia wachimbaji wadogo wa madini lakini wavuvi hawawezeshwi.

MTANZANIA: Pamoja na changamoto zilizopo katika jimbo lako ipi ambayo inakuumiza kichwa zaidi

AWESO: Kinachoniumiza zaidi kichwa ni barabara kwa sababu siku zote barabara ikiwa nzuri inafungua sekta zingine na itawavutia wawekezaji kuja kuwekeza hata katika kilimo cha miwa.

MTANZANIA: Ni mara yako ya kwanza kuwa bungeni, je umejifunza jambo gani katika Bunge hili la 11?

AWESO:  Unajua kabla sijaingia niliamini kuwa mule bungeni kuna wataalamu lakini cha kushangaza wakati mwingine tunajenga hoja ambazo hatuwatendei haki wananchi.
Tunatakiwa tusiwasahau wale waliotuamini na kushiriki mijadala kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Nilichojifunza zaidi, wabunge tumekuwa tukijikita kwenye itikadi kabla ya kutazama maslahi ya wananchi.

MTANZANIA: Nini ushauri wako kwa wabunge wenzake kuhusiana na hilo?

AWESO: Tukumbuke majukumu yetu kama wabunge kuwatetea wananchi waliotutuma bungeni.

MTANZANIA: Unakizungumziaje kiti cha Spika?

AWESO:  Unajua chochote ambacho anakifanya Spika wengine wanaona kama wanaonewa hata kama ni haki yao. 

MTANZANIA: Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ya baadhi ya watu kutekwa, nini maoni yako kuhusiana hilo?

AWESO: Mambo kama haya hatujazoea katika taifa letu kama wananchi tutoe taarifa pale wanapowagundua wahalifu.
MTANZANIA: Wakati bado hujawa mbunge ni mwanasiasa gani au mbunge gani aliyekuwa anakuvutia?

AWESO: Aliyekuwa ananivutia na kunihamasisha niwe mwanasiasa ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na mbunge aliyekuwa ananivutia ni marehemu Deo Filkunjombe (aliyekuwa Mbunge wa Ludewa).

MTANZANIA: Nini matarajio yako kisiasa kwa siku zijazo?

AWESO: Kwa umri wangu nahitaji kufanya siasa kwa muda mrefu, lakini huko mbeleni Mungu akijalia uzima natamani kuwa Katibu Mkuu wa chama siku moja. Navutiwa na utendaji kazi wa Katibu Mkuu wa sasa, Abdulrahman Kinana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles