27.6 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Aweso aorodhesha mafanikio ya Rais Samia sekta ya maji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita zaidi ya Sh bilioni 934.3 zimetolewa kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini.

Watumishi wa sekta ya maji wakimsikiliza Waziri wa Maji (hayupo pichani) alipokuwa akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Sekta ya Maji kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Wizara hiyo ina malengo ya kuimarisha huduma ya upatikanaji majisafi na salama kwa zaidi ya asilimia 95 katika maeneo ya mjini ifikapo mwaka 2025 na kwa vijijini kwa zaidi ya asilimia 85.

Takwimu za wizara hiyo zinaonesha hivi sasa upatikanaji wa huduma za maji umefikia wastani wa asilimia 72.3 kwa vijijini na asilimia 86 mjini sambamba na kukamilika kwa miradi 1,015 ya maji ambapo 915 ni ya vijijini na 100 ya mjini.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Sekta ya Maji kwa kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2022, amesema fedha hizo ni kati ya Sh trilioni 1.3 zilizoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini.

“Rais Samia alitupa maelekezo mahususi alisema hataki kusikia wala kuona Watanzania waishio mijini na vijijini wanateseka juu ya suala la maji, tumemsikia rais tunataka tuitoe sekta ya maji itoke kuwa ya malalamiko iwe sekta ya utatuzi,” amesema Aweso.

Aidha amesema miradi 463 ya maji imekamilika na kati ya hiyo 412 ni ya vijijini na 51 ya mjini huku upatikajani wa fedha za maendeleo ukifikia asilimia 74 hadi kufikia Januari 2022.

Waziri huyo amesema kupitia mpango wa taifa wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19 zimetolewa Sh bilioni 32.6 kati ya Sh bilioni 139.3 zilizoidhinishwa na kwamba kati ya fedha hizo Sh bilioni 12.069 ni kwa miradi ya mijini na Sh bilioni 20.6 vijijini.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akizungumza kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Sekta ya Maji kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kuhusu miradi inayotekelezwa katika Mkoa wa Arusha, Aweso amesema mradi mkubwa unaogharimu Sh bilioni 520 utekelezaji wake umefikia asilimia 80 na tayari wananchi wameanza kupata maji.

“Baadhi ya watu wa Arusha wamekuwa wakiteseka kutokana na athari za madini ya flouride, wamekuwa wakipinda miguu na wengine kuharibika meno Rais Samia ametupatia Sh bilioni 6 kuhakikisha watu wa Oldonyosambo wanapata majisafi na salama,” amesema.

Kwa mujibu wa Aweso mradi mwingine ni ule unaotekelezwa Longido ambao utekelezwaji wake umefikia asilimia 98 na kuahidi kabla ya Wiki ya Maji wananchi wa Namanga watapata maji safi na salama.

Wizara hiyo imejipanga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi iliyobainishwa na kushirikiana na sekta binafsi ili miradi husika ikamilike ndani ya muda uliopangwa.

Naye Meya wa Jiji la Arusha, Maximillian Iraghe, amesema wizara hiyo imepata mtu sahihi ambaye ataitoa kutoka mahali ilipo kwenda kwingine.

“Miongoni mwa wizara ngumu ni ya maji lakini wewe umeitendea haki kwahiyo nikupongeze, tumshukuru mheshimiwa rais kwa kuendelea kukuamini kuongoza wizara ya maji unafanya kazi nzuri,” amesema Iraghe.

Mbunge wa Arumeru Magharibi, Lembris Noah amesema; “Tukimaliza miaka mitano hakutakuwa na maswali kwa CCM kwa sababu ahadi nyingi zitakuwa zimetekelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles