AUSSEMS: WALETENI HAO KAGERA SUGAR

0
647
Patrick Aussems,

THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema wameshafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Kagera Sugar, unaotarajiwa kuchezwa Alhamisi, Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Simba itakutana na Kagera Sugar ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zake zote mbili za ligi hiyo dhidi ya JKT Tanzania 3-1 na mabao 2-1 walipocheza na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kagera Sugar ni timu pekee ambayo msimu uliopita iliweza kuifunga Simba katika mechi zote mbili, ikiwaliza Wekundu wa Msimbazi hao mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, kabla ya kuwatambia tena Uwanja wa Uhuru kwa kuwalaza bao 1-0.

Akizungumza jana baada ya kumaliza mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, Aussems alisema kikosi chake kimekamilika baada ya wachezaji wengine waliokuwa timu ya Taifa kurejea na sasa wanaendelea na maandalizi ya mwisho.

“Tumeshafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Kagera, nafahamu ni timu nzuri ila safari hii hatutakuwa tayari watufunge kwani tumejipanga kila idara,” alisema.

Alisema wanatarajia kuondoka kesho asubuhi kwenda Kagera, wakiwa na wachezaji 22, isipokuwa John Bocco ambaye ni majeruhi pamoja na Ally Salim akiwa timu ya Taifa ya vijana.

Aussems alisema kwa maandalizi waliyofanya, wanaamini Kagera Sugar hawatatoka mbele yao, wakipania kuwashikisha adabu wapinzani wao hao.

Akizungumzia kuhusu mshambuliaji wake tegemeo Meddie Kagere aliyekuwa anasumbuliwa na majeruha, Aussems alisema alikuwa akimfanyisha mazoezi mepesi ili awe fiti zaidi kwa sababu anamtegemea katika mchezo huo ukizingatia Bocco ni majeruhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here