Aussems ni dozi kwa kwenda mbele

0
447

Theresia Gasper -Dar es salaam

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, ameendelea kuonyesha kuwa hatosheki na mabao yanayofungwa na wachezaji wake katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo kuongeza dozi ili vijana wake waweze kucheka na nyavu zaidi.

Simba hadi sasa imecheza michezo minne, yote wakishinda wakianzia na JKT Tanzania (mabao 3-1), Mtibwa Sugar (2-1), Kagera Sugar (3-0) na Biashara United (2-0).

Licha ya kushinda mechi zote, Aussems ameonyesha kutoridhishwa na idadi ya mabao ambapo katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, alikuwa akiwanoa zaidi wachezaji wake katika ufungaji, huku akimwandaa kila mmoja kuwa na uwezo wa kucheka na nyavu.

Katika zoezi hilo, kila mchezaji alionekana kujituma zaidi hasa katika ukabaji pamoja na kusaka mpira na hatimaye kuitengeneza nafasi ya kufunga mabao.

Katika hilo, mshambuliaji tishio wa timu hiyo, Meddie Kagere, alionekana kung’ara zaidi na kufunga mabao manne, huku Ibrahim Ajib akitikisa nyavu mara tatu.

Akizungumza na Mtanzania, Aussems alisema kuwa kwa sasa atendelea kukinoa zaidi kikosi chake kwani bado ana muda mrefu wa kujiandaa kukabiliana na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaoatarajiwa kuchezwa Oktoba 23, mwaka huu, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Siwezi kuizungumzia kwa sasa Azam kwani bado tuna muda mrefu, hivyo tutaendelea kufanya programu tofauti tofauti ili timu yangu iwe fiti zaidi katika kupambana,” alisema.

Katika hatua nyingine, beki wa kulia wa timu hiyo, Shomari Kapombe, jana aliendelea kufanya mazoezi na wenzake licha ya kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.

Japo wachezaji walioitwa Stars walitakiwa kuripoti kambini jioni, wachezaji wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Mzamiru Yassin, Miraji Athuman, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Gadiel Michael, hawakuwapo katika mazoezi ya kikosi cha klabu yao zaidi ya Kapombe pekee.

Hata hivyo, Meneja wa kikosi hicho cha Msimbazi, Patrick Rweyemamu, alisema: “Wachezaji wengine walioitwa timu ya Taifa hawajaja wanaweza kuwa na programu nyingine, lakini Kapombe ameona ni kawaida kufanya mazoezi na wenzake kabla ya kuingia kambini jioni,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here