Malima Lubasha-Serengeti
MKAZI wa Kijiji cha Bisarara, Kata ya Sedeco, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Paulo Maseke (32), anadaiwa kumuua shemeji yake Esther Ryoba (28) kwa kumkata shingo kwa panga kutokana na ugomvi wa shamba.
Diwani wa Kata ya Sedeco, Raphael Matiko (CCM), amethibitisha kutokea mauaji hayo juzi.
Alisema kuwa wakati Esther akiwa analima shambani kwake, ghafla alikwenda shemeji yake na kuanza kugombana ikiwamo kutoleana lugha chafu.
Inadaiwa kuwa wazazi wa Maseke, na mkewe walikuwa na shamba lingine jirani na eneo yalipotokea mauaji hayo, ambapo walishuhudia mtoto wao akimkata kwa panga shemeji yake.
“Wakati tukio hilo linatokea na wazazi wa Maseke walikuwa shamba la jirani… Waliona tukio ikiwamo kukatwa kwa panga Esther, ambaye alivuja damu nyingi na hatimaye kufariki dunia,” alisema Diwani Matiko
Naye Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Mang’era Magesa, alisema kuwa kutokana na tukio hilo wazazi hao walifika ofisi kwake na kumjulisha kuhusu mauaji aliyofanya mtoto wao.
“Kutokana na taarifa hiyo, nilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walifika na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa,” alisema Magesa.
Mtendaji huyo wa kijiji alisema kuwa mtuhumiwa Maseke, amekuwa akijihusisha na matukio mbalimbali ambapo hivi karibuni alitoka Gereza la Butimba mkoani Mwanza kwa msamaha wa Rais Dk. John Magufuli. “Pia alikuwa na kesi ya kumchoma na kisu sehemu za siri mama yake mdogo,” alisema Magesa