31.9 C
Dar es Salaam
Sunday, January 16, 2022

Atumia swala ya Idd kueleza Mkapa aliyofanya kwa waislamu

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA 

SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu, amewaomba Watanzania kuzidi kufanya maombi ili Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, huku akitumia ibada hiyo kusema mambo ambayo Rais wa awamu ya tatu, marehemu Benjamin Mkapa, alifanya kwa waislamu. 

Akizungumza jana jijini hapa wakati wa ibada ya swala ya Eid El Hajj iliyofanyika katika Msikiti wa Gadaffi, Sheikh Rajabu alisema, moja ya kazi ya Mkapa ni pamoja na kujenga msikiti huo wa Gadaffi jijini Dodoma. 

Sheikh Rajabu alisimulia jinsi alivyokutana na Mkapa nchini Libya na kufanikisha ujenzi wa Msikiti wa Gaddafi. 

Alisema alikutana miaka kadhaa na marehemu Mkapa nchini Libya wakati huo yeye alikuwa akisoma nchini humo wakati Mkapa alifika kwa ajili ya kuiomba Serikali ya Libya kuwajengea Tanzania msikiti wa kisasa. 

Alisema Mkapa alifika nchini Libya akiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Musa Nkangaa wakiiomba Serikali ya Libya kujenga msikiti wenye hadhi Dodoma. 

“Tulikuwa vijana kadhaa ambao tulikuwa tukisoma kule nchini Libya, tulienda mpaka katika Hoteli ambayo alifikia (Mkapa) na tulikutana nae alishangaa kutukuta kule huku akisema yeye haelewi kitu kwani kila kitu kimeandikwa kiarabu. 

“Alipoitwa kwamba tumefika (hotelini), alishangaa kusikia kuna Watanzania kule, tulizungumza naye kwa kirefi, hakika alikuwa ni muungwana, alipeleka ule ujumbe na Libya wakakubali kujenga msikiti huu ambao ndio tunaswali hapa. 

Kadhi huyo wa Mkoa wa Dodoma alisema wakati Msikiti unakaribia kukamilika, marehemu Mkapa alifika na kukagua ambapo hakuridhishwa na sehemu ya kutawadhia akisema ipo juu hivyo aliagiza ivunjwe. 

“Hakuridhishwa na ile sehemu ya kutawadhia akaagiza kuvunjwe, alisema mtu mfupi kama yeye atachukuaje udhu katika sehemu ambayo ipo juu vile, hivyo tulijenga kwa chini kidogo na sehemu za kukaa kwa kila mtu wakati akitawadha,”alisema. 

“Mkapa alikuwa na mambo mengi sana, leo tunayaona na kusema sababu ameishafariki, mimi nasema akiwa hai Rais wetu John Magufuli ametupigania sana sisi waislamu na ndio maana sasa unajengwa ule msikiti mkubwa Jijini Dar es salaam, anachapa kazi iliyotukuka,”alisema. 

CHUO KIKUU CHA KIISLAMU CHA MOROGORO (MUM) 

Alisema jambo la pili ambalo analikumbuka kwa Mkapa ni kutoa jengo la umma la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Morogoro na kuwapa waislamu ili kiwe Chuo Kikuu cha Kiislamu. 

Alisema jambo hilo limeendelea kubaki katika kumbukumbu yake kwani marehemu Mkapa alikutana na wakati mgumu ambapo watu walihoji ni kwanini ametoa mali ya umma kwa waislamu. 

“Kauli yake kwamba mali ya umma inatoa kwa wenye umma, inaonesha kwamba alikuwa muungwana sana na sisi waislamu tunapaswa kuendelea kumuombea kwani hata vitabu vitakatifu vinatutaka kuwaombea kwa mazuri marehemu wetu,”alisema. 

AMANI UCHAGUZI 

Alisema kipindi hiki Tanzania ikielekea katika Uchaguzi Mkuu Watanzania wanapaswa kufanya maombi ili uchaguzi huo uweze kuwa wa amani na utulivu. 

“Wakati tukielekea katika Uchaguzi Mkuu hasa katika haya masiku 10 ambayo tunapashwa kuomba ambayo yanaisha leo (jana) tunapashwa kuomba kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ili uwe wenye heri, amani na baraka,”alisema. 

Pia aliwaombea wale ambao wamegombea nafasi mbalimbali Mungu aweze kuwafanyia wepesi ili waweze kushinda na wale ambao wameshindwa wakubali matokeo. 

AMANI, KUACHA MAOVU 

Aidha, Sheikhe Rajabu aliwaomba Watanzania kuzidi kuliombea taifa lizidi kuwa na amani kwani ndio mtaji wa kila jambo huku akisisitiza kuwa bila amani hakuna jambo ambalo litafanyika. 

“Haya makumi pia tuyatumie kuliombea Taifa liwe na amani, tuwaombee ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki lakini na sisi ni siku nzuri ya kula pamoja na kuwarehemu hao waliotangulia,”alisema. 

Vilevile,aliwaomba watanzania kuachana na matendo maovu na kumlilia Mungu katika kipindi hichi cha Sikukuu. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,583FollowersFollow
530,000SubscribersSubscribe

Latest Articles