25.9 C
Dar es Salaam
Sunday, December 4, 2022

Contact us: [email protected]

Athari za madudu ya ‘waziri’ Clinton zaanza kujitokeza

clinton-4KIWANGO cha uwezekano wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton kumrithi Barack Obama urais Januari 2017 kilikuwa kikubwa tangu wakati wa muhula wa kwanza wa Obama.

Kuna sababu kuu mbili za uwezekano huo; kwanza hakukuwa na mgombea mwingine maarufu na au aliyeonekana kuwa mwenye sifa zaidi kumshinda yeye miongoni mwa vigogo wa vyama vyote viwili shindani; Republican na Democratic anachotoka.

Sababu ya pili; baada ya Obama kuweka rekodi ya kuwa mweusi wa kwanza kuiongoza Marekani ilionekana wazi, wakati umefika pia taifa hilo kutoa rais mwanamke. Nani? Hakuna mwingine kama Clinton.

Alipotangaza kujiuzulu uanadiplomasa namba moja wa Marekani miaka zaidi ya minne iliyopita wakati Obama akijipanga kutetea kiti chake kwa muhula wa pili, licha ya kutoeleza sababu haswa ya kufanya hivyo, wengi walijua amelenga urais Novemba 8, 2016.

Ni baada ya kuukosa 2004 aliposhindwa na Obama katika mchuano wa kuteuliwa kuiwakilisha Democratic.

Kwa kujiweka kando na Obama, ulikuwa mkakati wa makusudi si tu kupata muda wa kujipanga na kujiandaa bali pia kuepuka kuharibu katika muhula wa pili wa Obama au kuepuka kuhusishwa na mabaya yatakayoukumba utawala wa Obama kama ilivyomtokea aliyetangulia, George W Bush.

Bush aliondoka madarakani akiwa chukizo kwa Wamarekani na anawekwa katika kundi la marais 10 wabovu kabisa katika historia ya taifa hilo na wakati wa uchaguzi wa 2004 wagombea wa chama chake walijiweka mbali naye.

Kwa bahati mbaya mikakati ya kujaribu kujiweka mbali na Obama umeonekana kutomsaidia mke huyo wa Rais wa 42 wa Marekani Bill Clinton.

Obama licha ya kuwa amebakisha miezi michache kumaliza muda wake, umaarufu wake bado uko juu kuliko wa Clinton na mpinzani wake katika kinyanganyiro cha urais Donald Trump.

Na hivyo, Clinton amejikuta akihitaji msaada wa Obama kumpigia kampeni katika uchaguzi huu.

Licha ya kufanya uangalifu asiharibu wakati wa utawala wa Obama, baadhi ya madudu aliyofanya wakati akiwa waziri yanaonekana kumvurugia.

Miongoni mwao ni suala la wahisani waliojitokeza kuichangia asasi ya familia yake ya Clinton Foundation, wanaodaiwa miongoni mwao ni ‘wahalifu’ waliotafuta kujenga ushawishi.

Anadaiwa pia kuzembea kilio cha ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya uliotaka kuimarishwa kwa ulinzi na matokeo yake yakashuhudia kuuawa kirahisi kwa maofisa kadhaa waandamizi akiwamo Balozi John Christopher Stevens.

Na fungakazi inayomuumiza zaidi ni kuibuliwa kashfa kuwa alitumia barua pepe binafsi katika masuala nyeti ilihali ikifahamika wazi kuwa njia hiyo ni hatari kwa usalama wa taifa.

Awali masuala mawili tajwa hapo juu alifanikiwa kuyapangua na hivyo akaendelea kubakia na umaarufu ijapokuwa ulishatikisika kwa tukio la Benghaz lililomfanya akabwe koo na mabunge ya Marekani yanayotawaliwa na wana- Republican.

Lakini aliendelea kupewa nafasi kubwa dhidi ya mpinzani wake, Donald Trump kabla na baada ya kura za uteuzi ndani ya vyama hivyo.

Lakini umaarufu wake ukashuka ghafla wakati Republican walipompitisha Trump kuwa mgombea wao katikati ya Julai, kabla ya kupanda tena wakati Democratic walipompitisha katika mkutano mkuu uliotajwa wenye mafanikio zaidi ya ule wa wapinzani wao.

Democratic walifanikiwa zaidi kwa vile waliweza kuunganisha makundi ya Clinton na ya aliyekuwa mpinzani wake katika kura za uteuzi Bernie Sanders.

Lakini sasa hali imebadilika, kura nyingi za maoni zinaonesha wagombea hao wakifungana au Clinton anaongoza kwa kura chache au anaburuza kwa Trump katika baadhi ya majimbo au kitaifa.

NINI KIMEBADILI MWELEKEO HUU GHAFLA?

Tuchukulie mfano wa kura ya maoni iliyoendeshwa karibuni na CNN/ORC zikiwalenga zaidi wapiga kura watarajiwa wa wagombea hao.

Kwa kuangalia mwenendo, lengo la timu ya kampeni ya Clinton ilionekana kuzifukuzia zile asilimia 51 ya kura shirika yaani za makundi ya kijamii alizopata Barack Obama mwaka 2012.

Ushirika huo wa kijamii ulihusisha mwitikio wa wapiga kura weusi, wenye asili ya Hispanic na vijana.

Lakini kuna kila dalili za wazi kuwa Clinton anaonekana kushindwa kuziteka ipasavyo kura hizo za Obama.

Mwitikio wa weusi na asilimia itakayopata Democratic unatarajia kuwa chini ya ule ambao Obama alipata wakati akitetea kiti chake cha urais mwaka huo.

Kura za maoni zinaonesha wapiga kura wenye asili ya Hispanic hawapendezwi sana wala kusisimuliwa na kampeni zake kuliko ilivyo kwa makundi mengine ya demographia.

Wapiga kura vijana, ambao wametengwa na Trump, hawavutiwi pia na Clinton. Anaonekana kukimbiwa na wapiga kura vijana wa kike na wa kiume waliokuwa wakimuunga mkono Sanders wakati wa kura za uteuzi.

Kura nne za maoni zinaonesha kwamba Clinton anaburuza nyuma ya zile asilimia 60 alizotwaa Obama miongoni mwa vijana wenye umri chini ya miaka 30 mwaka 2012.

Sehemu kubwa ya asilimia 20 ya vijana hao wameonekana kupendelea wagombea wa ‘chama cha tatu’; Gary Jonson wa Libertarian au Jill Stein wa Chama cha Kijani.

Kwa sababu hiyo mwitikio unaweza kuinufaisha Republican safari hii.

Na kura hizi kwa sehemu kubwa hazikupima athari ya kuanikwa kwa nyaraka zilizohusu kile alichohojiwa Clinton na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) wikiendi ile kabla ya Julai 4 mwaka huu.

Nyaraka hizo zilitolewa hadharani jioni ya Ijumaa iliyopita kabla ya wikiendi ya Siku ya Wafanyakazi nchini humo na hadi wakati huo ni kura mbili tu mpya za maoni kitaifa zilifanyika kuhusu suala hilo.

Wamarekani wengi waliohojiwa walisema hawana muda wa kuchimba kuhusu maelfu ya barua pepe zilizonaswa na Kamati ya Bunge kuhusu kilichotokea Benghazi.

Clinton mwenyewe alipoulizwa kuhusu mwandiko “C” katika nyaraka unachomaanisha, alisema pengine zinahusiana na kitu kama mfuatano wa alfabeti pamoja na kuwa katika nyaraka hizo hakukuwa na mfuatano huo wa alfabeti “A,” “B” au “D.”

Kwa wengi, mgombea huyo aliyekuwa akihesabiwa kuwa mwenye sifa zaidi ya kuwa rais wa taifa kubwa duniani, kuliko hata Obama, amedhihirisha namna alivyo ‘mjinga’ kuhusu namna serikali inavyofanya kazi pamoja na masuala ya usiri.

Kwa mujibu wa kura za maoni, asilimia zaidi ya 60 ya Wamarekani wanaamini kuwa Clinton si muwazi au mtu wa kuaminika.

Kwa walioyapitia mahojiano na FBI, Clinton ameonesha kwamba yu mwongo na mdanganyifu.

Wanasema kitendo cha FBI kumhoji bila kumrekodi na kuruhusu tu wasiri wake tu katika mahojiano, kunathibitisha shaka ya wengi kuwa kuna kitu kimefichwa.

Naam, mpinzani wake Trump amethibitisha kuwa na uwezo wa kujibomoa mwenyewe na wapiga kura wengi wataendelea kumwona hafai kuwa rais, lakini pia kwao Clinton asiyeaminika ni janga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,538FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles