Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Waajiri Tanzania (ATE) kimesema raia wengi kutoka China wanaoingia nchini, hawafuati sheria na masharti ya kuishi nchini ikiwamo kufanya kazi bila kuwa na vibali vya kazi. Kwa sababu hiyo chama hicho kwa kushirikiana na mashirikisho ya waajiri kutoka China, Norway na Kenya, kimetoa semina kwa kampuni za China zinazofanya biashara nchini kuhusu umuhimu wa kuwa na vibali vya makazi na kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa semina hiyo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka, alisema wageni wengi wanapewa vibali vya ukazi lakini wanapokuwa nchini wanaanza kufanya kazi au biashara.
Alisema mbali na elimu kuhusu vibali pia wametoa elimu kuhusu Sheria ya Kazi hususan kutoa mikataba bora sehemu za kazi. “Wageni wengi wanaokuja wanaomba vibali vya ukazi lakini baada ya kukaa kwa muda anaanza kujiingiza katika biashara na kazi bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo,” alisema Dk. Mlimuka na kuongeza: “Tumeandaa semina hii kwa wafanyabiashara na wafanyakazi wa China nchini kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu waweze kufanyakazi bila usumbufu”.
Alisema itahakikishwa Wachina wanakuwa na uelewa wa sheria na taratibu. ATE kwa kushirikiana na serikali ya Norway imechapisha Sheria ya Kazi na kanuni zake kwa lugha ya China, alisema.