Pretoria, Afrika Kusini
WATU wenye umri wa zaidi ya miaka 75 ambao hutumia Aspirin baada ya kupatwa kiharusi au maradhi ya moyo, wako hatarini kupata matatizo ya kuvuja damu tumboni, kwa mujibu wa Shirika la Utafiti wa Utabibu la Lancet.
Wanasayansi wanasema kupunguza athari hizo, watu wenye umri mkubwa wanapaswa kumeza dawa za kuzuia maradhi ya tumboni (PPI).
Lakini wamesisitiza kuwa Aspirin ina faida muhimu kama vile kuzuia maradhi ya moyo.
Utafiti wa utabibu Uingereza umeonyesha kwamba kutumia vidonge vya Aspirin kuna athari kubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa awali, hususan kwa watu wenye umri mkubwa.
Dawa hiyo ambayo inatumiwa kwa kiwango kikubwa kuzuia mshtuko wa moyo na maradhi ya kiharusi imehusishwa kwa siku nyingi kusababisha matatizo ya kuvuja damu tumboni.
Wataalamu hao wametahadharisha kuwa kusimamisha ghafla matumizi ya Aspirin kunaweza kuleta madhara, hivyo mtu yeyote anashauriwa kupata ushauri wa daktari ikiwa anatakiwa kubadili dawa.