27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

ASLAY & NANDY: MFALME NA MALKIA WANAOSUBIRI KUSIMIKWA

NA RASI INNO NGANYANGWA

YEYOTE anayehusika kutoa wazo la kuwakutanisha wawili hawa ili wafanye ‘kollabo’ anastahili kupewa tano manake amesoma vyema alama za nyakati kwenye Bongo Fleva, kutokana na kila mmoja wao kuwa katika kiwango kinachovutia tangu ‘Back’ walipojitosa kwenye gemu hadi ‘Front’ ya sasa.

Ingawa hawakuanza kwa nyakati sawia lakini kama kuna anayebisha kwamba kwa sasa ‘Mfalme’ Aslay na ‘Malkia’ Nandy wanafanya vyema kwenye tasnia, lazima atakuwa na kisokolokwinyo chake binafsi kwani chema hujiuza na kibaya hujitembeza.

Sikuwapa nyadhifa hizo kwa kuwa sitambui uwezo wa wengine, hapana, ila mnyonge mnyongeni haki yake mpeni kwani katika ‘Front’ waliyoamua kuvaa viatu vikubwa mno na kuweza kumudu saizi yake kwa kurudia wimbo ‘Subhalkheri’ inadhihirisha jinsi walivyokuwa na kiwango, ingawa ukubwa wa kiwango chao haukuanza kuonekana kwenye ngoma hiyo kwani tangu awali walishadhihirisha makali yao.

 ‘Ufalme’ wa Aslay unakuja kwenye kubadilisha fikra zilizoigubika Bongo Fleva kwamba kila wimbo lazima uwe wa kukimbizana, kila ngoma lazima iwe imegongwa kwa kulenga kuchezesha hata kama imeimbwa katika ‘Back’ hiyo ambapo nyimbo zilitengenezwa kwa ‘tempo’ ya kuchezwa kwenye shoo lakini kama mashabiki wanasikiliza maneno au hawasikilizi hilo halijalishi!

Lakini Aslay akaja na mbinu mbadala ya kurudisha masikio kwenye kuzingatia mistari inayoimbwa na vyombo vinavyopigwa kuwa kisindikizio cha maudhui halisi kama ambavyo unabaini ukisikiliza nyimbo zake. Malkia Nandy naye baada ya kustukia kuwa alikoanzia siko anakopaswa kung’ang’ania akajirudisha Uswazi, kwamba siyo lazima video ishutiwe kwenye mazingira ya bei mbaya ili ikubalike kwani kinachotakiwa ni mtiririko mwanana wa simulizi, engo sadifu za uchukuaji picha na msanii husika kugubikwa hisia zinazoshadadia anachokiimba ndicho alichokileta Nandy katika ‘Front’ ya sasa kwenye gemu na hakuna shaka kwamba, kama akiendelea kama anavyofanya sasa basi hakika Malkia mpya kwenye Bongo Fleva amepatikana.

Kwani kwa kawaida Mungu hakupi vyote lakini kuna watu amewapendelea kama ilivyo kwa Nandy, umbuji, sauti, mvuto hata matao yake si haba!

 Walichokifanya ndicho kinachotakiwa kwani hata mbele kwa wenzetu walikotuzidi kwa maendeleo ya kila kitu, kurudia nyimbo za zamani iwe kwa ujumla kamili au kwa kuchota baadhi ya vipande ili kunogesha ni mwafaka katika ‘Front’ ya sasa, kwani kuna ngoma huwa hazipitwi na wakati hata dahari kutokana na jinsi zilivyotengenezwa kama ambavyo Sabalkheri ulioimbwa na Sami Haji Dau na Mwapombe Hiari kwenye kundi la Culture Musical Club.

Ambayo tangu mwanzo imekonga na sasa imewafanya vijana watatu nikimaanisha Nandy, Aslay na Prodyuza Imma The Boy aliyeweka mkono wake kunadhifisha mikong’osio yake kadiri inavyotakiwa, wakikutanisha vizazi vya ‘Back’ kwa kukumbusha hisia na kupagawisha kizazi cha sasa kwa kuurudishia umaarufu wimbo huo hususan kwa vijana wenye uwezo kwenye sauti kama walivyofanya kwenye wimbo huo.

Mshawasha wa kuchota kwa Wahenga waliofanya vyema umeshika kasi kwa sasa ingawa ni kama umechelewa lakini kawia ufike kuliko kutofika kabisa na sasa ndiyo wakati umefika kwenye muziki wa Kizazi Kipya kwa kufanya kinachokubaliwa hata na watu wazima.

Walifanya onyesho la kipekee lenye mvuto mkubwa siku sita zilizopita pale kwenye fukwe za Escape One, Dar es salaam katika usiku wa mapenzi mubashara.

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,414FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles