Askofu Ruwa’ichi aanza mazoezi ya kutembea

0
1195

Aveline Kitomary -Dar es salaam

DAKTARI Bingwa wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (Moi), Profesa Joseph Kahamba, amesema Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Dar es Salaam, Yuda Ruwa’ichi ameanza kufanya mazoezi ya kutembea baada ya afya yake kuendelea kuimarika.

Askofu Ruwa’ichi alifikishwa Moi akitokea katika Hospitali ya Rufaa Kilimanjaro (KCMC) Septemba 9, mwaka huu saa tano usiku  ambako alifanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo na madaktari bingwa watatu ndani ya sasa tatu.

Profesa Kahamba aliiambia MTANZANIA Jumamosi jana Dar es Salaam kuwa kwa sasa Askofu Ruwa’ichi anaweza kutembea bila kuhitaji msaada wa mtu mwingine, pia ana uwezo wa kula chakula mwenyewe.

“Afya yake inaendelea vizuri, naweza kusema kuwa ufahamu umemrudia, anawatambua ndugu zake, watu mbalimbali anaongea nao vizuri tu, mpaka kufikia hatua ya kutembea ni dalili nzuri ya kupona kwake,” alieleza Profesa Kahamba.

Hata hivyo, alisema Askofu Ruwa’ichi bado yuko katika chumba cha uangalizi maalumu ambako jopo la wahudumu saba bado wanafuatilia afya yake kila baada ya saa moja.

Awali Profesa Kahamba alisema Askofu Ruwa’ichi anasumbuliwa na tatizo la damu kuvuja kwenye ubongo linaloitwa kwa kitaalamu ‘Chronic Subdural Hematoma’.

Profesa Kahamba alisema tatizo hilo linatokea mara baada ya mishipa ya damu kupasuka na damu kuvuja kwenye ubongo, huku sababu zikiwa ni kuumia sehemu ya kichwa, shinikizo la juu la damu la kupanda na matumizi ya dawa za maumivu.

Alisema hadi sasa watu mbalimbali, hasa viongozi wa dini walifika kumjulia hali huku kitabu maalumu kikiwa kimeandaliwa kwa wageni kuacha salamu zao kwani si wote wanaoruhusiwa kumwona.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here