31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU: KUNA DALILI MBAYA

Dk. Fredrick Shoo
Dk. Fredrick Shoo

Na Waandishi Wetu, DAR/MIKOANI

ASKOFU Mkuu  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amesema Taifa linakabiliwa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.

Amesema hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje kama njugu.

Mbali na hilo amesema pia Taifa limegubikwa na tatizo kubwa la rushwa inayosababisha baadhi ya wananchi kuonewa, kudhulumiwa na kukosa haki zao huku wengine wakilazimika kutumikia vifungo magerezani jambo ambalo ni hatari.

Askofu Dk. Shoo aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi katika ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini , Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika kipindi hiki ni vema Serikali ikawa makini na kujitahadharisha na tabia ya kuwamilikisha wawekezaji wa kigeni  maeneo makubwa kwani suala hilo limekuwa likisababisha migogoro mikubwa na wananchi jambo ambalo alidai ni dalili kubwa ya kutokea machafuko nchini ikiwa ni pamoja na kuwagawa Watanzania.

“Tuwe makini katika umilikishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji wa mataifa mengine jambo hili likiendelea hivi katika siku za usoni litatuondolea amani yetu kabisa.

“Ardhi ni kitu muhimu sana tusigawe kama Karanga, nchi yetu imekuwa na ukarimu wa kumilikisha wageni ardhi  ni tofauti sana na nchi nyingine na iwapo halitaangaliwa upya amani yetu tumeiweka rehani,” alisema.

Dk. Shoo alisema kwa sasa kumekuwa na vitendo vya uonevu vinavyoendelea nchini hali ambayo imekuwa ikisababisha baadhi ya watu kutopata haki kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutimiza wajibu wao kwa kusimamia haki na upendo kwa watu wote.

“Kuna watu wapo maabusu na magerezani leo kwa uonevu tu na kwa masilahi ya watu wachache, hawa wanaoonewa ipo siku watamlilia Mungu na awatawasikia ni vema tukaacha tabia ya kulipiza visasi,” alisema.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa Kanisa la KKKT, alisema ni vema mpango wa Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda utekelezwe kwa vitendo na kuacha siasa katika masuala ya maendeleo.

Kutokana na hali hiyo alisema ni vema mpango huo uende sambamba na utoaji wa elimu bora kwa Watanzani kwa lengo la kuzalisha wataalamu wa kutosha na kuacha kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi ili waje kuendesha viwanda.

Misamaha ya kodi

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk. Abedinego Keshmshara, ameiomba Serikali kuangalia upya masharti ya misahama ya kodi kwa taasisi za dini nchini kwani sasa kumekuwa na masharti magumu kwa wafadhili.

Kutokana hali hiyo wamesema ni vema Serikali ikapunguza masharti hayo  kwani taasisi za Wamisionari, zimeshindwa kuleta vifaa vya misadaa na badala yake wanaielekeza kwenye nchi nyingine zenye masharti nafuu.

Wito huo aliutoa jana mjini Bukoba, alipokuwa akitoa salamu za Krismas katika ibada ya kitaifa iliyofanyika mkoani Kagera.

“Tulipatwa na janga la tetemeko la ardhi,  lakini pamoja na yote tunaomba Serikali ipunguze masharti ya msamaha wa kodi.

“Wamishionari wengi ambao hujitolea wenyewe misaada lakini wanatozwa gharama kubwa siku hizi wanaamua kuhamia nchi zingine,” alisema Dk. Keshmshara.

Alisema tofauti na zamani ambapo waliweza kuwasilisha maombi yao hata katikati ya mwaka wa fedha wa serikali, hivi sasa wanatakiwa kuwasilisha kabla ya mwaka wa fedha wa Serikali kuanza.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristu Tanzania (CCT), Dk. Leonard Mtaita, Katibu Mteule, Mchungaji Moses Mtonya, aliomba Serikali kuweka utaratibu wa kukutana na viongozi wa dini zote ili kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwamo amani ya nchi.

Mkuu wa Mkoa

Naye Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu,  alisema Serikali itahakikisha misaada yote inayotolewa kusaidia waathirika wa tetemeko inaratibiwa na kusimamiwa vizuri.

“Tetemeko lilituletea madhara makubwa, limeacha majeruhi wapatao 140, vifo 17 na uharibifu wa mali, misaada tuliyopokea tutairatibu vizuri.

“Pia nawahimiza wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzitumia vema mvua za vuli na kuhifadhi vyakula kwani kuna upungufu wa chakula, tupande mazao ya muda mfupi,” alisema Kijuu.

ASKOFU PENGO

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewaasa Watanzania kuitunza amani iliyopo.

Akizungumza katika mkesha wa Sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Kardinali Pengo alisema amani haiwezi kuletwa na matajiri na watawala wa dunia.

Aliyasema juzi kwenye mkesha wa Sikukuu ya Krismas iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

“Usiseme mimi ni maskini siwezi kuwa chimbuko la amani, mimi ninayefanya kazi usiku na mchana ili kupata riziki nitawezaje kulete amani” alisema Kardinali Pengo.

  1. MALASUSA

Kwa upande wake A Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, alisistizxa kudumishwa kwa amani.

“Amani ndiyo msingi wa maisha ya mwanadamu hivyo niwatake waumini na wananchi wote kuwa mabalozi wa amani na upendo.

“Watu wapende kuonyesha upendo kwa wenzao ndio maana katika ibada ya leo tumepeana zawadi, hata kuja kwa Yesu Kristo ni zawadi kutoka kwa Mungu” alisema Dk. Malasusa.

WAKRISTO NA MAENDELEO

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Mhashamu Evaristo Chengula, amesema wakristo wanalo jukumu na haki ya kuchangia katika kuleta maendeleo nchini.

Askofu Chengula aliyasema hayo jana wakati wa ibada ya mkesha wa Christmas, iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki, Makatifu wa Antony wa Padua, lililopo jijini hapa.

“Lakini serikali haiwezi ikatufanya shule moja iwapokee watoto wengi zaidi ya uwezo wake, ama kufungua shule hakuna madawati,” alisema Askofu Chengula.

JPM NA KAZI

Katika hatua nyingine, Rais Dk. John Magufuli, amewatakia heri ya Krismasi waumini wote wa Jimbo la Singida na Watanzania wote kwa ujumla na amewasihi kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristu.

Dk. Magufuli amewahimiza Watanzania wote kuongeza juhudi katika kuchapa kazi kama alivyofanya Yesu kwani maeneo mengi ya nchi yameonekana kukabiliwa na uhaba wa mvua hivyo ni vema wakatumia vizuri mvua chache zinazoendelea kunyesha kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili kuepuka upungufu wa chakula.

Askofu Kinyunyu

Askofu Mkuu wa  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu amewataka Watanzania katika kipindi cha Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya kutojiingiza kwenye starehe na badala yake  wakae na familia kutafakari namna bora ya kufanikiwa katika mwaka 2017.

Askofu Kinyunyu alitoa kauli hiyo jana  alipokuwa akihubiri kwenye ibada ya sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika usharika wa kanisa kuu la (KKKT) Dodoma mjini.

Alisema kuwa inasikitisha pindi inapofikia sikukuu kama hizi walio wengi badala ya kutafakari na kumshukuru mungu kutokana na uzima aliowapa  wanajiingiza kwenye starehe zisizokuwa na tija.

Habari hii imeandaliwa na Faraja Masinde, Veronica Romwald , Leonard Mang’oha (Dar), Renatha Kipaka (Bukoba), Ramadhan Hassan (Dodoma), Janeth Mushi (Arusha), Upendo Mosha (Moshi) na Victor Bariety (Geita).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles