31.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU KILAINI AKUMBUSHIA MACHUNGU TETEMEKO KAGERA

ASKOFU METHOD KILAINI
Askofu Method Kilaini

NA ASKOFU METHOD KILAINI

“UTUKUFU kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema”. Huu ndio ujumbe unaotangaza kuzaliwa kwa mkombozi wetu Yesu Kristu.

Leo Watanzania tunaungana na Wakristo duniani kote kuadhimisha miaka 2016 ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu na mwokozi wetu.

Salamu salaamu ndiyo maneno yale  yaliyosikika mara ya kwanza siku ile alipozaliwa mwokozi wetu Yesu Kristo. Maneno haya yaliyoletwa na Malaika kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu, yakafika masikioni mwa mwanadamu yakasikika kama ifuatavyo: “Mimi nawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana”(Lk. 2:14)

SHUKRANI KWA MUNGU

Kristo Mwana wa Mungu nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu, Mungu alikuwa mwanadamu ili sisi tukombolewe.

Yeye ni mwanga alikuja kuleta mwanga penye giza, kuleta amani penye mafarakano, vita na mauaji, kufundisha upendo penye chuki, maadili penye ufuska, heshima penye uduni, maonevu na udhalilishaji, utu penye unyama.

Kristo alizaliwa ili sisi tupone. Kwa maandiko ya Injili ya Mt. Yohana bwana anatuambia: “Hapo Mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu … Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Yn. 1:1,14)

Krismasi ni sherehe kubwa kabisa tunapokumbuka tendo hilo la fumbo la ajabu, la upendo usio na kifani, upendo usio na mipaka wa Mwenyezi Mungu kwetu, upendo wa Mungu ulio zawadi ya pekee kwetu binadamu wote.

Upendo huo ni lile tendo lake Mungu la kuja kuwa sawa nasi na hata kuja kukutana nasi, kuja kuonana nasi, kuja kukaa nasi.

Tangu siku ile ya Noeli ya kwanza Mungu wetu si Mungu aliye mbali kabisa nasi, bali ni Mungu kati yetu, ni Mungu pamoja nasi, ni Emmanueli, yaani Mungu nasi.

Ni kutokana na upendo huo wa ajabu ndipo ujamaa wa binadamu umejenga wazo na utamaduni wa kupendana, kutoka, kusalimiana na kutakiana heri ya Noeli kwa kupeana zawadi.

Kama Mungu Mwenyezi alitupenda hata akajishusha kiasi hicho kwa sababu ya kutupenda, basi na sisi tufanye hivyo.

Kwamba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametulinda katika mwaka huu wote wa 2016 na tunatumaini kuingia mwaka wa 2017 na nguvu mpya. Ni wakati wa kuwashukuru wote waliotupa nguvu hata tukafikia siku hii ya Krismasi

KRISMASI NI SIKU YA FAMILIA

Bwana wetu Yesu Kristu alizaliwa katika familia takatifu, fukara lakini yenye upendo. Hii ilikuwa kutuonyesha kwamba familia ndiyo kitovu cha ukombozi wa binadamu, ndilo kanisa la nyumbani, ndiyo maskani ya utakatifu.

Mama Maria na Joseph walishiriki pamoja katika shida na vile vile katika furaha za kuzaliwa kwake Mwokozi. Kristo alitaka aje na alelewe katika familia.

Sikukuu ya Noeli, sikukuu ya Krismasi ni siku ya familia, baba, mama na watoto. Siku ya kujenga na kuimarisha familia katika shida na raha, katika shibe na upungufu, katika afya na magonjwa, katika ujana, utu mzima na uzeeni, katikati ya watu na wakiwa au wapweke.

Krismasi ni siku ya kusameheana, kurudiana kwa wale waliotengana, kuwajali watoto. Ndiyo sababu siku ya Krismasi huwa siku ya matashi mema, kadi, zawadi na furaha.

Watoto hupata zawadi hata kama ni kidogo lakini huwa ishara ya upendo. Pia wakubwa nao katika familia hupeana zawadi.

Familia imara hujengwa na watu wenye msimamo imara, yenye heshima kati yao, watu wenye maadili thabiti na watu wenye utawa, wacha Mungu na watu wa sala.

Maadili mazuri ndio msingi wa familia. Hakuna familia imara iliyojengwa kwa misingi ya wezi, wasema uongo, wapiga ramli, wazinzi au walagai. Hivyo hatuna budi ya kumwomba Kristo aliyezaliwa adumishe familia zetu.

Inasikitisha na kutia huzuni mkubwa sana kukuta familia inasambaratika, haina heshima, ikifanya vitu ambavyo hata mitaani havifanywi, kupigana, uhasama nakadhalika.

Hii ni jehenamu ambayo watu wawili na akili zao hujiingiza na hawataki kutoka au mmoja wao hataki kuona na kugeuka.

Anakuwa kama mwendawazimu au mvuta bangi. Inatisha kuona watoto wadogo ndani ya familia wanateseka katika chuki na uhasama wa wazazi wao.

Hilo ndilo ombi letu kubwa katika sikukuu ya kuzaliwa mwokozi, sikukuu ya Noeli, sikukuu ya Krismasi kwamba familia ziishi kwa upendo, kuheshimiana na kushikamana.

Inafurahisha sana kuwa na familia yenye uelewano kwa sababu pamoja hushinda changamoto nyingi. Familia hiyo hujua kwamba Kristo alizaliwa na kuwaletea heshima, akafa kuwakomboa na sasa ni wana huru wa Mungu.

Kristo alishinda mauti ya dhambi ambayo ndiyo adui mkubwa wa binadamu. Maovu na majanga mengi ya binadamu hutoka katika dhambi.

Dhambi inaanza hapo mtu anapojipenda mwenyewe na kusahau mwenzake, anaona furaha yake mwenyewe tu. Siku ya Krismasi ni siku ambayo familia husherehekea pamoja, hula pamoja na kushikamana kwa upendo.

KRISMASI NI SIKU YA MATUMAINI

Mwaka huu kitaifa sikukuu ya Krismasi itaadhimishwa wilayani Bukoba. Hii ni ishara kubwa na nzuri kwa sababu Septemba 10, mwaka huu Bukoba na Kagera kwa ujumla ilipata janga la tetemeko la ardhi.

Watu walifariki dunia, wengine walijeruhiwa huku nyumba kadhaa kuporomoka, nyingine zikapata nyufa kubwa na kuhatarisha maisha ya watu.

Hadi sasa bado kuna watu wanaishi katika mahema na kwenye mabaki ya nyumba hatarishi. Krismasi kuadhimishwa Bukoba ni faraja kubwa na ishara ya kuleta tumaini kwa watu.

Kujua kwamba katika Kristo tunashinda na tusikate tamaa hata kidogo. Tetemeko na majanga mengine si kaburi la kutufukia bali ni kengele ya kutuamsha ili twende mbele kwa nguvu na ari kubwa zaidi.

Tunawashukuru wote waliotusaidia katika janga hili. Serikali, mashirika na taasisi mbalimbali na watu binafsi. Kristo anayezaliwa katika siku ya Krismasi awazawadie. Tukiwa na mshikamano na upendo hakuna kisichowezekana. Kwa pamoja tutashinda.

Faraja na tumaini si tu kwa ajili ya watu wa Bukoba bali kwa wote wenye changamoto katika maisha.

Bwana wetu Yesu Kristo alete matumaini kwa wale ambao hawawezi, hasa wale wenye magonjwa sugu kama saratani na Ukimwi wajue kwamba katika Bwana wanakombolewa. Krismasi ni wakati wa kuwafariji, kuwajulia hali na kuwasaidia.  Kuwa na moyo mkuu Bwana yuko pamoja nawe akuokoe.

TULIOMBEE TAIFA LETU

Sasa tumemaliza mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano. Huu ulikuwa mwaka wenye changamoto nyingi, kusafisha mambo mengi na kupigana na rushwa, watumishi hewa, ulaghai, uzembe na kutowajibika.

Hii ni kazi nzito na ngumu kuifanya na inahitaji moyo na dhamira safi. Tumwombe Kristo aliyezaliwa ili sisi tupate wokovu atuepushe maovu haya, uovu wa rushwa, ulaghai na ufisadi ambavyo ni tunda la dhambi.

Hakuna nchi ambayo inaweza kuendelea kama kwanza haishindi vita dhidi ya rushwa.  Rushwa huzuia haki na kuleta uonevu, huvunja ari ya kazi na kukatisha tamaa. Rushwa ni mama wa kuvunjika amani.

Mtu hawezi kujiita Mkristo na akapenda rushwa ambayo ni adui wa ubinadamu ambao Kristo anatufundisha. Kama kuna rushwa majambazi yatashamiri kwa sababu yatalindwa; watu watakufa kwa sababu wasionacho hawatapata huduma, maendeleo yatakwama kwa sababu vyeo vitapatikana kwa rushwa si kwa uwezo. Viongozi wala rushwa bosi wao ni fedha hawajui mwingine. Ee.. Kristo tuokoe na rushwa.

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, msemo ulikuwa ‘Hapa Kazi Tu’. Hili linatukumbusha maneno ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorinto aliowaambia kwamba “Asiyefanya kazi na asile”. (2 Thes.3:6-15). Watanzania tunasifika kwa mambo mengi sana ukiwemo utulivu, amani, mshikamano, undugu na kupendana.

Lakini bahati mbaya hatusifiki kwa kutenda kazi. Mara nyingine mtu akiwa na kazi muhimu anamwajiri mtu kutoka nje ya nchi mwenye elimu ndogo kuliko ya Mtanzania kwa kigezo cha kuwa mchapakazi. Kweli sote tuitikie Hapa Kazi Tu! Kazi itatupa heshima, staha, amani na maendeleo.

Tunashukuru kwamba viongozi wetu wanatupa ujumbe unaoshabihiana na ujumbe wa Kristo aliyezaliwa kwa ajili ya wengine. Picha hiyo juu ya Mungu wetu wa Noeli, itupatie sote changamoto hasa kwa viongozi wetu.

Tunafurahi na tunatamani sana Serikali yetu iwe ni Serikali inayoshughulikia watu na kuhangaikia watu, iwe katika sera zake, sheria zake, mipango yake ya maendeleo na miradi yake.

Hata katika hali yetu ya umasikini tutasonga mbele kama tutatumia kile kidogo tukipatacho kwa ajili ya shida za watu, hasa raia wale wasio na ajira ya pekee na wale wa vijijini ambako ndiko maendeleo ya kweli yanaweza kupimwa.

Taifa ambalo wale wadogo wasionacho, wanaohangaika siku kwa siku wanathaminiwa na kusaidiwa wainuke na kuishi maisha ya heshima.

Tunashukuru na kuwapongeza sana wote wanaounga mkono sera ya kufanya kazi na kuwajibika. Hakuna riziki ya bure bila kufanya kazi.

Tunawapongeza wafanyabiashara, wasomi mbalimbali na walioajiriwa ambao wanajitahidi kufanya mipango ya kuwaendeleza Watanzania wengine katika nyanja mbalimbali.

Roho hiyo iendelee katika misingi ya uzalendo inayotuunganisha. Kwa roho ya ubinadamu, tunaweza tukalijenga taifa letu kwa kuchangiana katika upendo na ushirikiano.

Tuchangiane vipaji tulivyopewa na Mungu na tutaweza kutekeleza makubwa. Tuchangiane mali tuliyo nayo kwa lengo la kuleta maendeleo zaidi na si kwa anasa bali iwe kwa kusaidia familia zetu na vijana wetu.

Tumwombee Rais wetu, Dk. John Magufuli pamoja na viongozi wetu wote Mungu awape busara, ujasiri na nguvu za kutimiza mapenzi yake na kuwaletea wananchi maendeleo ya kudumu, upendo, uelewano na amani.

Tuliombee Taifa letu la Tanzania, Mungu atuneemeshe, atuepushe na majanga mbalimbali ili tuwe taifa lenye uzalendo na mshikamano. Tuwaombee vijana wapate ari ya kazi na kujituma, wajue kwamba maisha mazuri hutokana na jasho lao, kuishi kwa maadili mema na kushirikiana na wengine.

Tumwombe Mama Maria, Mama mwenye huruma, mama wa Mungu. Aliyemzaa mwokozi wetu Bwana wetu Yesu Kristo, alisema kwa dhati ‘mimi mjakazi wa Bwana’ awe mama yetu na atulee kama alivyomlea mwanawe Yesu Kristo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles